Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akionyesha moja ya Tuzo za ushindi kati ya nne za Kimataifa zilizotolewa kwa Benki ya NMB. |
Tuzo ambazo Benki ya NMB imeshinda kutoka majarida ya kimataifa. |
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kutangaza tuzo hizo. |
Tuzo hizi zinafanya jumla ya tuzo zote ambazo NMB imezipokea mwaka 2021, kufikia sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna amesema tuzo hizo ni matokeo ya Benki ya NMB kuwa rafiki kwa wateja wake.
Tuzo hizo ni pamoja na Tuzo ya Benki Bora ya Biashara na Benki Bora ya Huduma za Uwekezaji Tanzania mwaka 2021 zote kutoka Jarida la World Economic Magazine, Tuzo ya Benki Bora kwa Ubunifu wa Huduma za Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Banker na Tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Business.
Itakumbukwa mapema mwaka huu, Benki ya NMB ilitajwa kwa mara ya tisa mfululizo kuwa Benki Bora zaidi Tanzania na Jarida la kimataifa la Euromoney na Benki Bora ya wateja Binafsi kutoka Jarida la Global Banking and Finance. Hizi ni tuzo za juu kabisa za ubora zinazotolewa na majarida makubwa duniani yenye makao yake makuu jijini London na nchini Marekani.
Katika maelezo yake kwa wanahabari, Bi Zaipuna alisema tuzo hizo zimetolewa kwa kuzingatia vigezo kadhaa kwa benki vilivyopendekezwa vya ufanisi wa mahesabu na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na uwajibikaji wa benki katika jamii inayoizunguka. Leo hii, zaidi ya asilimia 93 ya miamala yote ya benki ya NMB inafanyika nje ya matawi ya benki.
Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki, mapato yatokanayo na mali za kampuni, uwiano wa fedha na gharama za uendeshaji, kiwango cha amana za wateja, Kiwango cha Mikopo katika soko, Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo isiyolipika, na uwiano wa hasara itokanayo na mikopo isiyolipika.
“Tuzo hizi zinadhihirisha nafasi ya uongozi wa Benki ya NMB katika sekta ya kibenki nchini. Jopo la majaji wa tuzo zote nne waliona kuwa huduma za kidigitali, suluhisho katika huduma za uwekezaji, pamoja na mchango wa benki katika jamii, zimechangia katika ushindi huo,” alisema Bi Zaipua na kuongeza:
Kwa miezi 12 iliyopita, Bi Zaipuna alisema “Benki imeendelea kuboresha huduma zake ili kufikia mahitaji ya wateja, hivyo kuziba pengo la huduma na suluhishi za kifedha sokoni.”
“Ni mafanikio makubwa kwa Benki ya NMB kupata tuzo sita mwaka huu. Tunajivunia kuwa juhudi zetu zinatambuliwa na hatutaacha kuwa wabunifu zaidi, tunatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kufikia viwango vya juu duniani na mwisho kuendeleza dira yetu ya kuwa benki inayoongoza na benki bora zaidi Tanzania.”
NMB imeendelea kuleta matokeo chanya kwa jamii za kitanzania kwa kuleta huduma zenye ubunifu wa hali ya juu na kuiweka jamii karibu zaidi kwa Benki hususan baada ya uzinduzi wa asasi ya kiraia ya NMB Foundation na Mpango wa Ufadhili wa masomo wa Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program kwa watoto wenye ufaulu wa juu kutoka kaya masikini.
No comments:
Post a Comment