Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday, 25 January 2021

WANAFUNZI WA KING'ONGO WAFURAHIA NEEMA YA MADAWATI KUTOKA BENKI YA NMB YENYE THAMANI YA MILIONI 40

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge (kulia) pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi King'ongo wakifurahi baada ya kukabidhiwa madawati 150 na Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa (kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akipongeza baada ya kukabidhiwa madawati 150 na Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa yaliyotolewa na Benki ya NMB wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi, King'ongo iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam. NMB imekabidhi shule sita zilizopo mkoa wa Dar es salaam madawati yenye thamani ya jumla Tzs 40 milioni.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge (kulia) akikabidhiwa madawati na Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa (kushoto) kwa ajili ya shule za msingi Makabe, Kimara, Kinyerezi Annex, Kibwegere na Mpiji Magohe sekondari yaliyotolewa na Benki ya NMB wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Msingi, King'ongo iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam. NMB imekabidhi shule sita zilizopo mkoa wa Dar es salaam madawati yenye thamani ya jumla Tzs 40 milioni.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi, King'ongo wakibeba madawati yaliyotolewa na Benki ya NMB wakati wa hafla iliyofanyika katika Shule hiyo iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Wazazi katika Kata ya King’ongo, wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam wamefurahia neema ya madawati yaliyopelekewa katika Shule ya Msingi King’ong’o pamoja na Sekondari kutoka Benki ya NMB na kusema watoto wao hawatakaa tena chini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi na wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo mbili, walisema kwa muda mrefu asilimia kubwa ya wananfunzi walikuwa wakikaa chini kutokana na uhaba wa madawati, hivyo msaada huo ni neema kubwa kwao.

“Makaratasi.. tupa kule.. visalfetii tuupa kulee,” walikuwa wakiimba wazazi hao wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge akipokea madawati 150 kwa ajili ya shule ya King’ongo kutoka Benki ya NMB.

“Kwanza tunamshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kutupazia sauti hadi sasa tunaona vyumba vya madarasa vinajengwa, maana yake msongamano wa wanafunzi utapungua; lakini pia tunaishukuru Benki ya NMB kwa msaada huu wa madawati, hatimaye watoto wetu sasa suruali na sketi zao zitabaki salama maana walikuwa wakikaa chini kwenye makaratasi na matofali huku wengine wakikaa kwenye visalfeti,” alisema Salma Said mmoja wa wazazi ambao watoto wao wanasoma katika Shule ya Msingi King’ongo.

Awali, Mkuu wa Mkoa Kunenge wakati akipokea msaada huo alisema NMB wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam, wanahakikisha masuala ya afya, elimu na mambo mengine ya kijamii yanatimia kwa kufuata utashi wa Rais Dk. John Magufuli.

“Leo tumepokea madawati 400 kwa ajili ya shule nne za Wilaya ya Ubungo, miongoni mwa shule hizo ni hii ya King’ongo ambayo itapata madawati 150 pia kuna ukarabati na utanuzi wa vyumba vya madarasa unaendelea kwa agizo la Rais Magufuli,” alisema Kunenge.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Isaya Makore alisema NMB wamekuwa karibu nao wakati wote walipowahitaji katika kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za masuala ya afya na elimu, hata katika suala la Shule ya Msingi King’ongo wameonyesha mfano bora.


“Kumekuwa na mshikamano mkubwa katika kukamilisha ujenzi huu wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi King’ongo tangu Rais Magufuli atoe neno, NMB ahsanteni sana na endeleeni na moyo huu wa kizalendo,” alisema Makore.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa alisema suluhu kwa changamoto za sekta ya elimu Tanzania kwa NMB ni kipaumbele, wanatambua kuwa elimu ni nguzo kuu ya maendeleo kwa taifa lolote duniani.

“Ingawa serikali inafanya mengi na makubwa, sisi wadau tuna wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii na tumeweka sera ya uwajibikaji kwa jamii ambapo asilimia moja ya faida baada ya kodi hutumika kwa misaada kwa jamii,” alisema Baragomwa na kuongeza:

“Tunatambua wateja wetu wanatoka katika jamii, tunaposema NMB karibu yako ni karibu yako kweli. Ndiyo maana leo tumetoa madawati 400 kwa Wilaya ya Ubungo ambapo kati ya hayo madawati 150 tunayakabidhi kwa ajili ya Shule ya Msingi King’ongo ili wanafunzi wawe na mazingira bora ya kujifunza.”

No comments:

Post a Comment