- Wabunifu wa mifumo ya computer (wasanidi) sasa wanaweza kuunganisha mifumo yao katika mfumo wa M-Pesa kwa urahisi na kwa haraka.
- Kufunguliwa kwa M-Pesa API kunaongeza fursa ya ubunifu kwa ajili ya kuleta huduma za malipo zinazokidhi mahitaji ya mtumiaji.
Vodacom M-Pesa, mfumo wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi unaoongoza nchini umepitia katika mabadiliko mbalimbali kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, ikiwemo uhamisho wa kihistoria na uboreshaji kwenda kwenye mfumo wa kizazi cha pili (second-generation platform) ambao una ufanisi wenye kasi, usalama zaidi na wa kisasa, na cha muhimu zaidi mfumo huu unaendeshwa hapa hapa Tanzania ili kurahisisha matengenezo. Tangu hapo mfumo huu umepata sifa mbalimbali na kutambuliwa kimataifa ikiwemo kujipatia cheti cha ithibati kutoka taasisi ya kimataifa inayosimamia kampuni za mawasiliano (GSMA).
Akiongea na wasanidi (developers) na wadau wa teknolojia za mifumo ya fedha (Fintech ecosystem stakeholders) Hisham Hendi, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC amesema kufunguliwa kwa API za M-Pesa App ni hatua nyingine ya kuhamasisha uvumbuzi katika nyanja za teknolojia ya huduma za kifedha na biashara za kidijitali nchini.
"Tukiwa ni kampuni yenye ndoto ya kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali, tunaunga mkono ubunifu wa mifumo ya kidigitali kwa ajili ya kuunda mifumo itakayobadilisha maisha ya watu, na ndio maana sasa tumefungulia API za M-Pesa ili kurahisisha biashara zenu na watengenezaji wa programu kuunganisha mifumo mingine na mfumo wa M-Pesa na kuwaruhusu kufanya majaribio yatakayoonesha aina mbalimbali za uwezo wa ziada katika mfumo ambao matokeo yake utaleta mabadiliko ya kweli nchini," alisema Hendi.
Kuwekwa wazi kwa API za M-Pesa kunakamilisha bunifu nyingine kadhaa zilizofanywa na Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC, hizi ni pamoja na kuanzishwa kwa huduma ya Lipa kwa Simu, huduma hii ya ushirikiano inawezesha mteja kulipia huduma bidhaa kwenda M-Pesa akitokea mtandao wowote na benki yeyote nchini, Huduma ya kutuma Fedha Kimataifa (IMT) na M-Pesa App ambazo zote zina kusudi la kutengeneza jamii ambayo haitumii fedha taslimu na kuleta uchumi wa kidijitali.
"Miundombinu thabiti ya maendeleo inawezesha biashara kufanyika kwa uhuru pamoja na watengenezaji wao wa mifumo na programu mbalimbali na pia kufungua fursa ya ubunifu katika kutengeneza mifumo ya malipo kwa uhuru kabisa, kutengeneza mfumo wa malipo unaokidhi mahitaji yako bila kutushirikisha sisi moja kwa moja," alibainisha Hendi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom M-Pesa Epimack Mbeteni amesema kwamba API mpya zilizozinduliwa leo zinakuza uzoefu wa kidijitali kwa watumiaji, jambo ambalo linarahisisha uunganishaji wa mifumo ya malipo katika mfumo wa huduma za kifedha wa M-Pesa uwe rahisi, wa haraka na wenye ufanisi zaidi.
Alitoa wito kwa watengenezaji wa programu za computer (developers) kutumia fursa hii kutengeneza programu mpya kwa ajili ya kutoa huduma ya biashara kwenda kwa mtumiaji (business-to-consumer), Mtumiaji kwenda kwenye biashara (consumer-to-business) na Biashara kwenda kwenye biashara nyingine (business-to-business) ambayo itaweza kuunganishwa katika mfumo mkuu wa malipo.
"Kuzinduliwa kwa API za M-Pesa sasa kutawezesha wabunifu na waundaji wa mifumo kuweza kujaribu kile wanachobuni katika mifumo yetu, lakini pia tunatumaini kwamba tutaona mawazo mengi mapya, programu na biashara mbalimbali zikiunganishwa na mfumo wetu mkubwa kwa ajili ya kutoa huduma zilizoboreshwa zaidi kwa wateja" alihitimisha.
Wateja na watumiaji wa mwisho watanufaika kutokana na ubunifu wa watengenezaji wa programu kutokana na kupata huduma za malipo ambazo zinaendana na huduma husika. Vile vile inafungua uwezekano wa kuleta ubunifu zaidi wa kutengeneza huduma za kipekee ambazo zinahusiana na M-Pesa.
Uzinduzi wa API za M-Pesa ni kielelezo muhimu cha jitihada zinazofanywa na kampuni ya Vodacom Tanzania PLC za kujenga jamii ya Kidijitali kwa kuhamasisha ubunifu katika teknolojia ya fedha (fintech) na mifumo ya malipo nchini.
No comments:
Post a Comment