Serikali imeipongeza Benki ya Biashara ya DCB pamoja na Asasi ya Uyacode kwa kuanzisha ushirikiano uliowezesha uanzishwaji wa miradi ya kilimo, ufugaji, viwanda vidogovidogo kwa wanavicoba walio chini ya asasi hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa miradi hiyo katika kijiji cha Malivundo katika wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani jana, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji alisema wengi wa wanufaika wa miradi hiyo ni wananchi wenye vipato vya chini na kati itakayowawezesha kuwainua kiuchumi na hatimaye kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa kila mmoja wao na kwa Taifa kwa ujumla.
Katika hotuba hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, B. Beng’i Issa Naibu Waziri alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli kupitia Wizara ya Fedha ilifanya maboresho mbalimbali kwenye Sekta ya Fedha ikiwa ni pamoja na kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na baadae kufuatiwa na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2019 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha hivyo VICOBA vilitambuliwa kama taasisi rasmi zinazoruhusiwa kutoa huduma ndogo za fedha kwa wanachama wake.
“Leo tukiwa tunazindua miradi hii ya Kilimo cha kisasa, Ufugaji wa kisasa na Viwanda vidogovidogo kwa Wanachama wa UYACODE inaonesha ni jinsi gani asasi hii ilivyoweza kutumia fursa zilizopo kutokana na Serikali yetu kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara nchini.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Benki ya Biashara ya DCB kwa kuingia makubaliano ya ushirikiano na UYACODE kwa ajili ya kutoa huduma za kibenki kwa wajasiriamali wadogo wadogo kwani fedha hizi za watanzania walioamua kupiga hatua za kujikwamua kiuchumi zinahitaji usalama mkubwa na huduma zenye masharti nafuu.
“Ninafahamu Benki ya DCB inatoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo hivyo naamini wanachama wa UYACODE watanufaika na huduma hii ya mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji yao kwa gharama nafuu na hatimaye kuweza kujikwamua kiuchumi na nina imani ushirikiano huu kati ya DCB na UYACODE utakuwa na faida za kiuchumi kwa pande zote mbili kwa maana ya wanachama wa UYACODE kwa upande mmoja na kwa DCB kwa upande mwingine”, alisema Naibu Waziri Kijaji.
Pamoja na hayo alisema serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha kwa gharama nafuu miongoni ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha riba kinachotozwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa benki za biashara zinapokopa BoT kutoka asilimia 16 Mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 5 Mwaka 2020 hivyo kuzitaka taasisi zote za kifedha na hasa benki za biashara ikiwemo DCB kujielekeza katika utoaji wa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wananchi hususan wakulima na wafugaji wadogo wadogo ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawakopeshwi na mabenki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa alisema DCB wanaamini kutoa fursa zenye tija kwa wateja wao na kwa watanzania kwa ujumla wakijikita katika kutoa huduma na bidhaa za kimkakati zenye tija kwenye soko zinazotoa wigo mpana kwa wateja wao.
Alisema Kwa miaka kadhaa DCB imewekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma zinazowalenga wajasiriamali walio katika vikundi mbalimbali wakiwa na vikundi vya Vicoba zaidi ya 500, huduma ambazo zimeweza kubadilisha maisha na kukuza mitaji ya wengi ya wanavicoba hao.
“Vikundi hivi vinanufaika na huduma bora za kibenki na zenye masharti nafuu za DCB kwa kupitia akaunti maalumu za Vicoba, baadhi ikiwemo masharti nafuu ya kufungua akaunti, masharti nafuu katika upatikanaji wa mikopo, masharti nafuu katika uendeshaji wa akaunti hizo na mengineyo.
“Tumefarijika sana kuona miradi hii ya kilimo cha kisasa, Ufugaji wa kisasa na Viwanda ikizinduliwa, hili ni jambo jema sana kwa wanachama wa UYACODE, tunawaahidi DCB tutakua bega kwa bega na wanachama wa UYACODE kuweza kulifanikisha hili”, alisema Bwana Ndalahwa.
Mkurugenzi huyo alisema anaamini ushiriano huo utakuwa chachu ya mafanikio ya kiuchumi kwa wanakikoba zaidi ya 10,000 wa UYACODE na kwa DCB.“
Niwaahidi DCB itaendelea kuwa bega kwa bega katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Magufuli katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kiuchumi katika kuboresha huduma zake na pia kuanzisha huduma zinazokidhi mahitaji halisi ya huduma za kibenki kwa watanzania”, aliongeza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Uyacode, Michael Mgawe ALISEMA Uyacode imekuwa ikipata mafanikia mbalimbali ikiwemo mshikamano na upendo miongoni mwa viongozi na wanachama miaka 18 hadi sasa, kutoa mafunzo imara kwa vikundi vya vicoba visivyovunjwa mwisho mwa mwaka, utoaji wa mikopo na kudhamini mikopo ya vikundi na wanavicoba mikopo ya magari, bajaji, pikipiki, mashine za kusaga na kukoba na pia kuweka mifumo mizuri ya makusanyo ya michango na marejesho ya mikopo katika vikundi vyao ikiwemo pia mradi wa mafunzo ya vicoba katika mikoa mbalimbali 21 bara na visiwani baada ya kupata kibali kutoka Wizara ya Tawala za Mikoa za Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
No comments:
Post a Comment