Picha ya pamoja kutoka kushoto Anorld Kisukuli Mkurugenzi wa kanda ya kati Dodoma wa chama cha kutetea Abiria Tanzania, RTO mkoa wa Singida Edson Mwakihaba na Neema Temba. |
Singida, Februari 28, 2020 – Ikiwa ni sehemu ya kuiunga mkono Serikali katika kupambana na ajali za barabarani, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imetoa darasa juu ya masuala ya usalama barabarani kwa waendesha boda boda mkoani Singida chini ya kampeni yake ya ‘Usinywe na kuendesha chombo cha moto’
Kampeni hiyo ya nchi nzima, inalenga kuwaelimisha watumiaji wa barabara na haswa madereva juu ya unywaji wa kistaarabu ikiwa ni hatua muhimu inayochukuliwa na kampuni hiyo kutokomeza ajali zinazosababishwa na unywaji usio wa kistaarabu.
Katika kipindi cha mwaka mmoja kampeni hii imefanyika katika mikoa nane ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Tanga, Arusha, Moshi na Iringa ikiwafikia zaidi ya watu 100,000.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika kwenye stendi ya mabasi mkoani Singida, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Singida,Edson Mwakihaba alisema kwa kulishirikisha jeshi la Polisi kampuni ya SBL imeiunga mkono serikali katika kuelimisha umma juu ya unywaji wa kistaarabu na kusisitiza umuhimu wa kutatua tatizo hilo.
Mwakihabaalisema baadhi ya madereva hunywa kiasi kikubwa cha pombe pasipo kujali madhara yanayoweza kusababishwa na kitendo hicho na kuonya kuwa vitendo vya aina hiyo vinaweza kusababisha ajali mbaya.
“Sote tunafahamu kuwa matumizi ya vileo yana uhusiano mkubwa na uendeshaji mbovu ambao unaweza kusababisha ajali mbaya za barabarani zenye athari kubwa kwa jamii zetu. Athari zake siyo tu zinawagusa watumiaji wa vilevi bali hata maisha ya wengine na kusababisha upotevu wa maisha na ulemavu kwa watu ambao wangeweza kuchangia uchumi wa nchi,” aliongeza.
Alisema pamoja na kusababisha vifo visivyotarajiwa na majeraha, unywaji usiokuwa wa kistaarabu una maadhara makubwa kwenye sekta ya afya kwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kwa ajili ya huduma, madawa na vifaa tiba kwa waathirika wa ajali za barabarani na hivyo kuwa ni mzigo kwa Serikali.
“Ajali hizi pia ni mzigo kwa vyombo vyetu vya utekelezaji wa sheria kwa kuwa maofisa wanalazimika kuzishughulikia wakati zinaweza kuzuilika ambazo zinasabishwa na madereva wanaondesha wakiwa wametumia vilevi,” aliongeza.
Akizungumzia namna kampeni hiyo itakavyoisadia jamii aliongeza, “sote kwa pamoja ikiwamo sisi Polisi, madereva, jamii na wadau wengine tuna jukumu la kutafuta suluhisho la kumaliza tatizo la kutumia vilevi na kuendesha vyombo vya moto. Ninayo furaha kuona SBL pamoja na kwamba biashara yao ni kuuza vilevi, wameona wanawajibu wa kuhimiza unywaji wa kistarabu”.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Meneja Uhusiano na Serikali wa SBL Neema Temba alisema kampeni ya unywaji wa kistaarabu inalenga kuielimisha jamii kuwa wanywaji wanapaswa kunywa kwa kiasi na kuhakikisha unywaji wao hauna madhara kwao na kwa watu wanaowazunguka.
“SBL imedhamiria kuungana na serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa jamii na haswa madereva ambao wanakunywa na kuendesha vyombo vya moto wanaelimishwa juu ya madhara ya vitendo hivyo na kutakiwa kubadilisha tabia zao,” alisema.
Kwa taarifa zaidi wasiliana na;
John Wanyancha
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma-SBL
Simu: 0692148857
E-mail: john.wanyancha@diageo.com
No comments:
Post a Comment