Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Tuesday, 18 August 2026

NBC YAITIKIA WITO WA RAIS SAMIA, YASISITIZA DHAMIRA YA KUCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto), akimsikiliza Meneja wa NBC Tawi la Zanzibar, Bw. Abdul Karim Mkila (anayeshika kipaza sauti), akieleza kuhusu huduma na suluhisho mbalimbali za kifedha zinazotolewa na benki hiyo kwa wananchi na wafanyabiashara wa Zanzibar. Rais Samia alipata fursa ya kutembelea banda la NBC wakati wa Maonyesho ya Biashara yaliyofanyika sambamba na Tamasha la Kizimkazi, Zanzibar, lililohitimishwa mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi (kulia), akizungumza na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto), wakati wa hafla ya kuhitimisha Tamasha la Kizimkazi lililoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika Kizimkazi, Zanzibar, mwishoni mwa wiki. NBC ilikuwa miongoni mwa wadau na wafadhili muhimu walioshiriki katika kufanikisha tamasha hilo, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuunga mkono shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji nchini.

Zanzibar | Agosti 16, 2026

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuwa mshirika wa kimkakati katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, ikiahidi kuendelea kuwawezesha wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na ongezeko la uwekezaji, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa sekta ya utalii.

Benki hiyo imesema itaendelea kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zitakazowawezesha wafanyabiashara kupata mitaji, kupanua shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kuwekeza katika fursa mpya za biashara, hususan katika maeneo yenye kasi ya ukuaji wa kiuchumi, ikiwemo Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla.

Akizungumza kufuatia hitimisho la Tamasha la Kizimkazi mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, alisema benki hiyo inaona fursa kubwa katika mabadiliko yanayoendelea Zanzibar na imejipanga kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha fursa hizo zinageuka kuwa shughuli endelevu za kiuchumi.

“NBC itaendelea kuwa mshirika wa wafanyabiashara na wawekezaji katika kutumia fursa zinazopatikana Zanzibar, ikiwemo eneo la Kizimkazi. Tumejipanga kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zitakazowasaidia kupata mitaji, kukuza biashara zao na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa maeneo haya,” alisema Bw. Sabi.

Alisema uwezeshaji wa kifedha ni sehemu muhimu ya kujenga mazingira yanayowezesha sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, kwa kuwa ukuaji wa biashara una uwezo wa kuongeza shughuli za uzalishaji, ajira na fursa za kipato kwa wananchi.

Kauli hiyo ya NBC imekuja wakati ambapo Zanzibar, hususan maeneo ya Kusini, yanaendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za kiuchumi zinazochochewa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na maendeleo ya miundombinu.

Akihitimisha rasmi Tamasha la Kizimkazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zinazozidi kujitokeza Zanzibar, akieleza kuwa mabadiliko yaliyofanyika, hususan katika Wilaya ya Kusini, yamefungua nafasi kubwa zaidi kwa shughuli za biashara na uwekezaji.

Rais Samia alisema eneo hilo limepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita, akibainisha kuwa ongezeko la uwekezaji, hususan katika sekta ya utalii, limekuwa miongoni mwa vichocheo muhimu vya mabadiliko hayo.

“Wilaya ya Kusini imepata mabadiliko makubwa sana ikilinganishwa na mwaka 2016 kutokana na kuongezeka kwa fursa za biashara zilizotokana na uwekezaji, hususani kwenye maeneo ya utalii. Tamasha la Kizimkazi limekuwa chachu muhimu kuelekea mafanikio hayo. Hivyo, tunawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hizi,” alisema Rais Samia.

NBC YAUNGA MKONO WITO WA RAIS SAMIA

Akizungumzia wito huo wa Rais Samia, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa NBC, Bw. Elvis Ndunguru, alisema kauli hiyo inaweka msisitizo kwenye nafasi ya sekta binafsi katika kuendeleza mnyororo mpana wa thamani unaotokana na ukuaji wa utalii.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na biashara za huduma, usafirishaji, malazi, chakula na vinywaji, bidhaa za ndani, burudani, sanaa na huduma nyingine zinazohusiana na utalii.

“Kwa upande wetu, dhamira ya NBC ya kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji ipo wazi na inaakisi umuhimu wa upatikanaji wa huduma na mitaji inayowawezesha wadau wa sekta binafsi kuchangamkia fursa hizo na kuzifanya kuwa shughuli za kibiashara zenye tija na endelevu,” alisema Ndunguru.

NBC YASHIRIKI TAMASHA LA KIZIMKAZI

NBC ilikuwa miongoni mwa wadau walioshiriki kikamilifu katika Tamasha la Kizimkazi, ambapo ilishiriki katika Maonyesho ya Biashara yaliyotoa fursa kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuonyesha bidhaa, huduma na shughuli zao.

Zaidi ya hayo, benki hiyo ilidhamini hafla maalum ya mnada wa sanaa za picha ulioongozwa na Rais Samia, ambao ulilenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na uhifadhi wa mazingira.

“Ushiriki wetu katika shughuli hizo unaonyesha namna tulivyolenga kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za kifedha kwa kushirikiana na wadau katika masuala yenye umuhimu kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira,” aliongeza Ndunguru.

Katika hafla hiyo, Rais Samia aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuchangia kufanikisha Tamasha la Kizimkazi, akiwemo NBC kwa mchango wake katika kufanikisha shughuli za tamasha hilo.

NBC imeendelea kusisitiza kuwa uwezeshaji wa sekta binafsi kupitia huduma na mitaji ni sehemu muhimu ya kuchochea ukuaji wa biashara, kuongeza ajira na kukuza shughuli za kiuchumi, huku ikiangazia fursa zinazojitokeza Zanzibar kutokana na uwekezaji na ukuaji wa utalii.

Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa muhimu kuhusu sekta ya benki, fedha na biashara Tanzania.

No comments:

Post a Comment