Wafanyakazi wa Benki ya NBC wakifurahi baada ya kufanyika uzinduzi wa Club ya biashara Mkoa wa Tanga. |
Aidha benki hiyo imeendesha mafunzo ya kibiashara kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati kwa lengo pia la kuwaongezea uwezo, uelewa na ubunifu katika ufanyaji wa biashara zao.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Klabu hiyo ya Biashara mkoani Tanga juzi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara NBC, Elvis Ndunguru alisema kuwa benki hiyo imedhamiria kurahisisha huduma za kibenki kwa makundi mbalimbali hususani wafanyabiashara ambao ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi nchini.
Alisema kuzinduliwa kwa klabu hiyo ya Biashara kunafanya klabu za biashara katika benki hiyo kuwa tisa nchini huku malengo yake yakiwa ni kuwaunganisha na kuwakutanisha wafanyabishara pamoja ili kutafuta fursa za ufanyaji wa biashara na kubadilishana uzoefu.
Ndunguru alisema klabu hizo za biashara zimekuwa sehemu ya wafanyabiashara kupata masoko na kuongeza kuwa katika kuhakikisha benki inachangia ukuaji wa sekta ya biashara nchini, imeamua kuanzisha vilabu hivyo vya wafanyabiashara (NBC B Clubs) ili kukuza na kuimarisha biashara nchini.
"NMB B Club ni mahali muafaka pa kuelimisha wafanyabiashara juu ya masuala mbalimbali kuhusu biashara na tangu kuanzishwa kwa klabu hizi za biashara, wanachama wamekuwa wakinufaika na mafunzo mbalimbali ikiwemo jinsi ya kutumia vitabu vya mahesabu, elimu ya masoko na pia elimu ya mlipa kodi kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato nchini TRA," alisema na kuongeza.
"Klabu hizo zimekuwa zikipanua masoko kwa wafanyabiashara, kwa mfano kwa miaka minne mfululizo sasa tumekuwa tukipeleka wafanyabiashara China na mwaka huu tunatarajia kuwapeleka Ujerumani kwa sababu kuna maonesho ya viwanda lakini pia tunafikiria kupeleka watu Ulaya na Marekani kwa ajili ya kukutana na wenye viwanda na wanaotengeneza mashine mbalimbali jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wetu," alisema
Alisema mfanyabiashara akiwa mwanachama wa klabu hizo atapata unafuu wa tiba katika mikopo inayotolewa na benki, anayeweka amana kuweza kupata riba kubwa zaidi na wanaobadilisha fedha za kigeni kupata punguzo katika gharama za kubadilisha fedha.
Kuhusu mafunzo ya Biashara alisema waliamua kuyatoa baada ya kuona kunauhitaji na umuhimu wa wafanyabiashara kupata uelewa ili kupunguza kupata hasara na kudanganywa na watendaji wasiowaaminifu.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Maheji ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa klabu hiyo aliipongeza NBC kwa kuamua kufungua klabu na kutoa elimu ya mlipakodi, utunzaji wa kumbukumbu na jinsi ya kuweka mahesabu sawa.
“Niipongeze NBC kwa uzinduzi wa klabu hii na kutoa mafunzo haya kwani moja ya eneo ambalo wafanyabiashara wengi wanakosa ni hili la utunzaji wa taarifa za biashara zao yaania kumbukumbu, hivyo niimani yangu kuwa litapunguza sana migogoro kati ya wafanyabisha na Serikali hasa TRA wakati wa ukadiriaji wa kodi zao’ alisema Maheji.
Kwa upande wake Ofisa Mkuu Msimamizi wa Kodi kutoka TRA makao makuu, Julius Mjenga alisema wafanyabiashara wanapaswa kuwa makini katika kutunza kumbukumbu za biashara ili kuepusha migororo na TRA hasa wakati wa ukadiliaji wa kodi.
"Napenda kuwaambia wafanyabiashara kwamba ili waweze kukadiliwa kodi zao vizuri ni muhimu watunze kumbukumbu zao, hata hivyo changamoto kubwa inayoonekana kati ya TRA Na wafanyabiashara ni kulalamikia makadirio ya kodi sasa ili hii iondoke watunze kumbukumbu zao," alisema
Naye Kaimu Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Tanga, Liberati Macha alisema wamekuwa walitoa mikopo kwa wajasiriamali wanaoanza na kuendelea na biashara hivyo watu wasisite kuja kuchukua kwani vigezo ni kuwa na mradi halali unaoendeshwa kwa mujibu wa utaratibu unaotambulika kisheria.
Kwa upande wake mfanyabiashara ambaye ni mteja wa NBC aliyenufaika na klabu za biashara, Haji Mambo alisema kupitia klabu hizo wameweza kuunganishwa na watu mbalimbali duniani ambapo yeye alifanikiwa kwenda China na kuonana na wafanyabiashara wengine waliombadilisha mawazo na mitazamo katika biashara zake.
No comments:
Post a Comment