Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo mbalimbali vya habari leo tarehe 31 Januari 2020 na iliyochapishwa katika magazeti kwa mujibu wa sharia za benki kuu, utendaji wa benki umeendelea kuimarika ikilinganishwa na mwaka uliotangulia huku ufanisi katika nyanja zote muhimu ukiongezeka kwa kiwango cha kuridhisha.
Akiwakilisha taarifa za fedha za robo ya nne ya mwaka 2019, mkurugenzi wa Fedha wa benki ya DCB Ndugu Zacharia Kapama, ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ukuaji wa mizania ya benki, ambao umechagizwa na ukuaji wa amana za watejakwa asilimia 14 (Shilingi bilioni 10.1), ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Ukuaji wa amana umeisaidia benki pia kuongeza ukuaji wa mikopo ambapo benki imefanikiwa kuongeza kiwango ghafi cha mikopokwa asilimia 11 (shilingi bilioni 8.0), ambacho ni kiasi kikubwa ukilinganisha na ongezeko la mikopo katika miaka miwili iliyotangulia. Mikopo ghafi ya benki imekua kutoka shilingibilioni 90.5mwaka 2018 kufikia shilingibilioni 93.3mwaka 2019.
Ili kufikia kiwango hiki, benki imefanikiwa kutoa mikopo mipya kwa wateja wake kinachofikia shilingi bilioni 60, huku shilingi bilioni 18zikiwakilisha mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), na Shilingi Billioni 10 ikiwakilisha mikopo ya wanawake na vijana. Benki pia imeendelea kutoa mikopo kwa sekta mbalimbali zikiwemo sekta binafsi za biashara, elimu afya na ujenzi.
Akielezea upatikanaji wa faida, Ndugu Kapama ameainisha kuwa ukuaji wa faida, ukiachilia mbali kuchangiwa na ukuaji wa mizania, pia umechagizwa na ongezeko la mapato yasiyotokana na riba baada ya benki kufanikiwa kukuza idadi ya wateja wake kutoka 175,000 mwaka 2018 kufikia wateja 194,000 mwaka 2020. Ongezeko hili limeongeza idadi ya akaunti za amana na miamala ya kibenki, huku wateja wakifurahia huduma za kidijitali bila kwenda matawini.
Kwa kuongezea, ufanisi wa benki umeongezeka hasa katika usimamizi wa matumizi ya riba na yasiyo ya riba. Benki imefanikiwa kudhibiti ukuaji wa matumizi yasiyo ya riba, huku ikihakikisha huduma kwa wateja zinaboreshwa. Benki pia imefanikiwa kudhibiti ongezeko la riba kwa wateja na kuhakikisha wateja wanapata thamani bora ya huduma zake bila kuathiri ukuaji wake.
Katika taarifa hiyo, Ndugu Kapama pia ameainisha upunguaji wa mikopo chechefu ya wateja kutoka asilimia 19 mwaka 2018 kufikia asilimia 13 mwaka 2019. Hii imetokana na juhudi za benki kuhakikisha kuna ufanisi na usimamizi madhubuti katika utoaji mikopo na ukusanyaji madeni. Benki itaendelea na juhudi za kuhakikisha mikopo chechefu inafikia kiwango kinachokubalika na wadau wa sekta ya fedha mnamo mwaka huu wa 2020.
Katika miaka yake takriban 17 ya uendeshaji, benki ya DCB imeweza kukuza idadi ya matawi kutoka tawi moja na kufikia manane (8) hadi mwaka huu wa 2019. Pia imekuza idadi ya wateja kufikia 194,000. Ukuaji huu umechangia benki kupata faida mfululizo tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2015, na imekuwa ikitoa gawio kwa wanahisa wake katika kipindi chote cha miaka 12.
Hapo mbeleni, benki ya DCB, inatazamia kukuza mizania yake kwa kutumia fursa za ukuzaji biashara na ina azimia kutumia ipasavyo fursa na njia mbadala za utoaji huduma kwa wateja kupitia mitandao, wakala wa kibenki, na upanuzi wa mitandao ya matawi na vituo vidogo vya huduma ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa utengenezaji wa mapato kupitia njia ya mapato yasiyo ya riba.
- Benki ya DCB ndio benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam huku ikiwa ndio benki pekee iliyokua kutoka benki ya wananchi/jamii (community bank) na kufanikiwa kuwa benki ya biashara (commercial bank)
- Benki ya DCB imefanikiwa kukuza mtandao wa matawi yake kufikia manane huku ikifungua tawi Dodoma na inaendelea na mchakato wa kufungua matawi na vituo vya huduma (service centers) katika mikoa mingine na imefungua mtandao wa mawakala na huduma za kijiditali hadi kufikia mawakala zaidi ya 700 nchini nzima.
- Benki imefanikiwa kuongeza mtaji wake kupitia soko la hisa kwa miaka yote 18 huku ikipata faida mfululizo na kujiimarisha kibiashara. Hivi sasa benki inao uwezo wa kutoa mikopo mikubwa zaidi na ya muda mrefu kwa wateja
- Benki imefanikiwa kuzindua mfumo wa akaunti za kidijitali ambapo umeiwezesha kuhudumia wateja wengi zaidi na kuwafikia hadi wale wa vijijini. Hii imeongeza ukuaji wa mapato na ongezeko la idadi ya wateja na ufanisi katika utoaji huduma
- Benki imefanikiwa kuzindua huduma na bidhaa mpya kwa wateja wake ambazo ni Lamba kwanza (Fixed deposit), Akaunti ya Skonga, DCB sokoni, pamoja na garantii za wakandarasi zisizo na dhamana wakati wa kuomba tenda.
- Tumeboresha huduma ya mikopo ya nyumba ujenzi wa nyumba kwa kuongeza ushirikiano na Tanzania Mortgage Refinancing Company
- Tumeongeza ufanisi wa huduma ya mikopo kwa ushirikiano na taasisi ya ushauri FSDT, hivyo kufanya huduma ya utoaji mikopo kwa wateja kuwa ya haraka Zaidi.
- Benki imeboresha gharama zake kwa kuondoa gharama katika akaunti za community kama vikoba, akaunti za miradi ya serikali, na akaunti za wastaafu. Hii imepelekea kuongeza idadi kubwa ya wateja ambao wengi ni wa kipato cha cha chini na cha kati.
Mawasiliano: Simu Namba: +255 22217201; Barua Pepe/Tovuti: info@dcb.co.tz; www.dcb.co.tz
No comments:
Post a Comment