Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkutano wake hivi karibuni. |
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi akizungumza na Wanahabari na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) hivi karibuni. |
Kaimu Mkurugenzi wa Ubunifu, Bi. Magreth Ezekiel (kulia), akiwasilisha ripoti ya miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa Mhe William Lukuvi. |
Waziri Lukuvi, amesema kuwa Shirika linapaswa kuingia katika mfumo wa kidijitali wa utunzaji wa kumbukumbu za wapangaji na taarifa zao, na taarifa hizi zifanane na za NIDA. Amesema kuwa katika taarifa hizo, NHC inapaswa kujua jina kamili la mpangaji, anafanya nini, mwajiri wake nani, anwani zake na kila kitu.
Ameongeza kusema kuwa NHC inapaswa kufanya uhakiki huu wa kuwatambua wapangaji wake haraka iwezekanavyo kabla ya mwezi Marchi mwakani zoezi hili liwe limekamilika. Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi, ameitaka NHC kufanya upya uhakiki wa majengo yaliyokuwa ya Msajili na yaliyojengwa na NHC.
Katika Mkutano wake huo ulioishirikisha Menejimenti ya Shirika, Waziri Lukuvi, ameitaka pia NHC kutumia wataalamu wake wa ndani na nje wanaoweza kukaa pamoja na wabia kuangalia Serikali inapata faida inayokusudiwa, kwani haiwezekani NHC itoe thamani kubwa ya viwanja vyake halafu wanapata faida ndogo ya asilimia 25 na mbia apate faida kubwa ya asilimia 75 bila kujua wao wameingia gharama kiasi gani za ujenzi. Amesema kuwa kuendesha miradi ya ubia mia moja na tisini na mbili (192) ambayo Shirika imeingia na watu binafsi, mikataba hii mingi haina tija ya moja kwa moja kwa NHC.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi, amelitaka Shirika kuhakikisha kwamba wateja wote waliouziwa Nyumba na Shirika wanapatiwa hati ili waweze kuwajibika kulipa Kodi ya Ardhi ya Serikali. Aidha, amelitaka Shirika kuhakiki nyumba zote zilizotaifishwa kwa kutumia gazeti la Serikali ili kuona umiliki wake kwa kuwa ana amini baadhi ya nyumba zimeingia kwenye mikono isiyo salama.
Waziri Lukuvi, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa ubunifu wa kujiendesha lenyewe kwani sasa NHC haikopi tena fedha kutoka kwenye mabenki bali inatumia fedha zake za ndani katika kukamilisha miradi yake mbalimbali. Pia ametoa salamu za pongezi kwa NHC zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, kwa Shirika kutoa gawio la shilingi milioni mia saba hamsini na kwamba ni matarajio yake kwamba Shirika litaongeza kiwango cha gawio kwa Serikali katika mwaka ujao.
No comments:
Post a Comment