Mkuu wa kitengo wa Wateja Rejareja, Masika Mukule (katikati) akizungumza kwenye hafla hiyo. |
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Mahusiano na Mawasiliano wa benki ya KCB, Christina Manyenye alisema wameanza kuwapeleka China wafanyabiashara hao ambao ni wateja wa benki hiyo ili wakakutane na wazalishaji halisi na si walanguzi au madalali ambao huwauzia bidhaa kwa bei ya juu. Alisema kwa muda mrefu wafanyabiashara nchini ambao wanakwenda China wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo za lugha na kuuziwa vitu bei za juu hivyo kupitia safari hizo wanazoziandaa mambo hayo hayatajitokeza.
“Tatizo kubwa ambalo wafanyabiashara walikuwa wanakutana nalo ni kuuziwa vitu kwa bei ya juu na walanguzi au madalali sasa kupitia safari hii tutawakutanisha na wale wazalishaji halisi ambao wanaviwanda ambapo watapata fursa ya kutembelea viwanda vyao kisha kutoa oda za kutengenezewa bidhaa zao.
Lakini pia kuna tatizo la lugha kule, kupitia safari hii tuliyoiratibu sisi KCB Benki tutawapatia wakalimani ambao watatembea nao kila mahali ili kurahisisha mawasiliano yao na wazalishaji hao,” alisema.
Naye Meneja Uhusiano wa Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Moses Kisaka alisema wana matumaini kwamba siku hizo 10 wafanyabiashara hao wataweza kuzunguka na kukutana na wazalishaji pamoja na kutumia fursa hizo kufanya manunuzi ya bidhaa zao. Alisema wafanyabishara hao watakutana na wazalishaji halisi watakaowauzia vitu kwa bei ya chini kuliko ilivyokuwa awali walipokuwa wakienda wenyewe na kukutana na walanguzi waliokuwa wanawauzia vitu kwa bei ya juu.
“Tunafanya hivi kwa lengo la kuwasaidia wapunguze gharama za kupata bidhaa, tunaamini safari hizi zitakuwa ni muendelezo na tunatumaini mwakani kuwapeleka wafanyabiashara wengi zaidi,” alisema. Aidha alisema benki hiyo imeanzisha kitengo cha KCB Biashara Club kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara mbalimbali na kuzungumza juu ya changamoto na fursa za kibiashara wanazokutana nazo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa wafanyabiashara wanaoenda China, Saada Sipemba alisema safari hiyo itawasaidia kupata fursa ya kuona maonyesho makubwa yanayofanywa na wenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo vyombo vya ndani pamoja na mashine. “Pia itatuwezesha kwenda kujifunza na kukutana na wazalishaji wenyewe bila kupitia kwa madalali wowote hivyo itatusaidia kununua bidhaa kwa bei nafuu na kuja kuziuza nchini kwa bei nafuu pia,” alisema Sipemba.
Kuhusu Benki ya KCB
Benki ya KCB ni benki kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati iliyoanzishwa mwaka 1896 kisiwani Zanzibar. Toka hapo benki imekua na kuenea katika nchi za Tanzania, Kenya Sudani ya Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na Ethiopia. Leo hii ina mtandao mkubwa zaidi katika kanda hii ikiwa na matawi 262, mashine za kutolea fedha (ATM) 962, na wakala 15,000 wanaotoa huduma za benki masaa 24 siku saba za wiki Afrika Mashariki.
Benki ya KCB imesajiliwa katika soko la hisa la Nairobi, Dar es Salaam, Uganda na Rwanda. KCB Bank Group pia linamiliki kampuni ya bima ya KCB, KCB Capital na KCB Foundation. Nchini Tanzania, KCB ilifungua milango yake mwaka 1997 na toka hapo imekuwa mdau mkubwa katika kukuza sekta ya fedha nchini. Kwa sasa benki ina matawi 14 Tanzania bara na visiwani Zanzibar. Matawi hayo ni Samora, Mlimani, Uhuru, Msimbazi, Lumumba, Buguruni, Oysterbay, Mbagalajijini Dar es Salaam; Moshi, Zanzibar, Arusha Main na TFA, Mwanza na Morogoro.
Benki ya KCB Tanzania ni mlipa kodi mzuri, mwajiri wa watanzania zaidi ya 300, inafundisha wafanyakazi wake weledi wa kikazi na pia pale inapotokea nafasi inapeleka wafanyakazi katika soko la Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment