Dar es Salaam, Septemba 18, 2019: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya uwakala wa huduma za kibenki na Shirika la Posta nchini ili kupanua wigo wa huduma za benki hiyo sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini.
Hatua hiyo inatajwa kuwa itaongeza wigo wa mtandao wa utoaji huduma za kifedha kwa njia ya kijiditi huku ikienda sambamba na azma ya serikali ya kupanua ushiriki wa wananchi katika shughuli za kifedha (financial inclusion).
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa kutoa huduma za kubeki kati ya Posta na NBC jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema kupitia mtandao wa ofisi za Shirika la Posta nchini lenye mtandao wa matawi 370, kutaiwezesha Benki ya NBC kuwafikia maelfu ya wananchi nchi nzima katika utoaji wa huduma zake za kibenki kwa gharama nafuu.
“Ushirikiano huu kati ya NBC na Posta utawezesha ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya serikali kwa urahisi zaidi. Kwani ulipaji wa kodi na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatafanyika katika mazingira salama na rafiki kwa wananchi kupitia ofisi za Posta. Wafaidikaji wa ushirikiano huu kati ya NBC na Posta sio tu wateja bali watakuwepo wastaafu, wanafunzi, wakulima, wazazi, na wafanyabiashara.’’ Alisema
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema ushirikiano huo utawawezesha kutumia mifumo ya kidijitali na wingi wa ofisi za posta katika kutoa huduma za kibenki nchi nzima.
“Kwa sasa NBC ina mawakala wapatao 2,000 na hivyo kuungana na Shirika la Posta, kupitia mtandao wa ofisi zake 370, kutatuwezesha kuongeza idadi ya wananchi watakaofikiwa na huduma za kibenki kwa ukaribu.’’ alisema
Aliongeza kuwa ushirikiano huo, ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa mabenki ya kupeleka huduma ya kifedha kwa wananchi hasa walioko mikoani na vijijini.
Kwa upande wake Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe alisema kwa kuanza shirika hilo na NBC wataanza kutoa huduma katika ofisi 99 zilizo maeneo mbalimbali nchini.
“Huduma hizi ni zile zote za kibenki, kukusanya mapato ya serikali, kuhamisha na kutuma fedha, kufungua akaunti pamoja na huduma nyingine za kibenki.
“Katika kuimarisha shirika kibiashara na kurahisisha wananchi wapate huduma kwa ukaribu shirika tayari linashirikiana taasisi kadhaa ikiwemo Benki ya Posta, Necta, MSD, Tanesco, NIC, mifuko ya hifadhi ya jamii, mashirika na makampuni mbalimbali,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta nchini Luteni Kanali Mstaafu Dk. Haroun Kondo alisema kulingana na mageuzi ya kimfumo na maboresho mbalimbali yanayofanywa sasa na shirika hilo, yatatoa nafasi bora kwa taasisi na makampuni mbalimbali kuvutiwa kuweka ofisi au kuingia ubia wa kutoa huduma au uwakala wa huduma zake.
No comments:
Post a Comment