Januari 29, 2019 - Benki ya biashara ya DCB imefanikiwa kupata faida ya shilingi bilioni 1.9 katika mwaka 2018 huku ikiipiku hasara ya shilingi bilioni 6.9 iliyopatikana mwaka 2017 ambayo inawakilisha ongezeko la asilimia 463.
Benki imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha inatoka kwenye hasara iliyopata mwaka 2017 na kurudi kwenye faida. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni kupitia na kuboresha ufanisi wa mfumo wa uendeshaji biashara ambapo gharama za uendeshaji zimeshuka huku huduma mpya za kidigitali zimeanzishwa, huduma hizi zimevutia wateja wengi zaidi kufungua akaunti za amana. Juhudi zilizopelekea upatikanaji wa faida mwaka 2018;
- Mapato halisi ya riba kuimarika kutokana na utoaji mikopo katika sekta mbalimbali na kuchangia ongezeko la mikopo ghafi kutoka shilingi bilioni 88.6 mwaka 2017 hadibilioni 90.6 mwaka 2018. Mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 65 imetolewa mwaka 2018 ambapo kati yake, shilingi bilioni 21 ni mikopo ya wajasiriamali wadogo.
- Kuboresha ufanisi katika mfumo wa uendeshaji biashara kupitia mfumo wa kidijitali huku mkazo ukiwekwa katika kuongeza amana za gharama nafuu kupitia bidhaa za amana za kidijiti na usimamizi wa mizania wenye ufanisi. Gharama za amana zimeshuka kutoka shilingi bilioni 9.8 mwaka 2017 kufikia shilingi bilioni 6.8 mwaka 2018.
- Kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni yatokanayo na mikopo chechefu na hivyo kupunguza tengo la mikopo chechefu kutoka shilingi bilioni 4.5 hadi shilingi milioni 263.
- Kuongeza mkazo katika ufanisi wa utendaji na kuchangia upunguaji wa gharama za uendeshaji kutoka bilioni 21.2 mwaka 2017 kufikia shilingi bilioni 16.9 mwaka 2018.
Huduma za kidigitali zimekuwa chachu ya kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji na gharama za riba. Hizi ni mathalani akaunti ya kidijiti (DCB Digital Account), DCB Kibubu Digital Account, DCB FDR Digital account. Account hizi zinamuwezesha mteja kufungua akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, Kutunza pesa na kuwekeza kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Idadi ya wateja imeongezeka kutoka 144,475 mwaka 2017 kufikia 175,204 mwaka 2018 na hivyo kuchangia ongezeko kubwa la miamala ya kibenki ambapo mapato yasiyo ya riba kuimarika katika mwaka 2018.
Benki ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa kama Benki ya Jumuiya ya Wananchi “community bank” na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kufuatia kilio cha wakazi wengi wa Jiji kutokuwa na njia rahisi ya kupata mitaji midogo midogo ya biashara. Benki ya DCB imekuwa ni benki ya kwanza kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa mwaka 2008, na imeweza kukuza mtandao wake wa matawi kufikia matawi nane likiwepo tawi la Dodoma, na inatarajia kuongeza matawi mengine mikoani katika miaka ya mbeleni.
No comments:
Post a Comment