Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 4 December 2018

WAZIRI MPINA, VODACOM FOUNDATION WATOA MAFUNZO NA VIFAA VYA UOKOAJI ZIWA VICTORIA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina (wa pili kushoto) akipokea moja ya jaketi maalum la kujiokoa (life jacket) kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation Bi. Rosalynn Mworia ikiwa ni moja ya vifaa mbalimbali vya uokoaji vilivyotolewa na taasisi hiyo mwishoni mwa wiki hii mjini Ukerewe. Waziri Mpina alitangaza kuanza kwa ujenzi wa bweni kwaajili ya wanafunzi wanaoishi upande wa pili wa kivuko ambapo taasisi ya Vodacom Foundation iliahidi kutoa vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi hao. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Bw Cornel Magembe (wa kwanza kushoto) na muasisi wa taasisi ya Sukos Kova Foundation, Bw Suleiman Kova.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina akipokea radio za upepo (Radio Calls) kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation Bi. Rosalynn Mworia ikiwa ni moja ya vifaa mbalimbali vya uokoaji vilivyotolewa na taasisi hiyo mjini Ukerewe ili kukabiliana na majanga ya majini. Waziri Mpina alitangaza kuanza kwa ujenzi wa bweni kwaajili ya wanafunzi wanaoishi upande wa pili wa kivuko ambapo taasisi ya Vodacom Foundation iliahidi kutoa vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi hao. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Bw Cornel Magembe (wa kwanza kushoto) na muasisi wa taasisi ya Sukos Kova Foundation Suleiman Kova.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh Luhaga Mpina akikabidhi mtungi wa kuzimia moto (fire extinguisher) kwa wawakilishi wa shule ya sekondari Mibungo baada ya kupokea vifaa mbalimbali vya uokoaji kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation Bi Rosalynn Mworia mwishoni mwa wiki hii mjini Ukerewe. Waziri Mpina alitangaza kuanza kwa ujenzi wa bweni kwaajili ya wanafunzi wanaoishi upande wa pili wa kivuko ambapo taasisi ya Vodacom Foundation iliahidi kutoa vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi hao. Wanaoshuhudia ni muasisi wa taasisi ya Sukos Kova Foundation Suleiman Kova na Bi Rosalynn Mworia.
Ili kuokoa zaidi ya wanafunzi 1,300 wanaosafiri kwenye maji kila siku asubuhi kwenda shule katika visiwa vya Ukerewe jijini Mwanza, Waziri wa Uvuvi na Mifugo Luhaga Mpina amesema serikali itajenga bweni ili wanafunzi hao waishi shuleni.

Waziri Mpina alitangaza uamuzi huo wakati akipokea Msaada wa vifaa mbalimbali vya uokozi majini vilivyotolewa na Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Sukos Kova Foundation ambao pia wametoa mafunzo ya uokozi na kujikinga na majanga kwa wanafunzi, walimu, wavuvi na wakazi wengine wa visiwa hivyo.

Msaada huu unajumuisha makoti ya kujiokolea 1,568, vifaa vya kuzimia moto 21, mablanketi ya kuzimia moto 21, pamoja na vifaa vya kutolea huduma ya kwanza 21 ikiwa na malengo ya kusaidia shule za sekondari na msingi kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pindi yanapotokea. Pia simu za redio 8 pamoja na suti za majini 20 zimegawiwa kwa viongozi wa fukwe za maji.

“Nawashukuru sana Vodacom Tanzania Foundation kwa msaada huu ambao utawaweka salama wanafunzi wa shule hizi, lakini pia wakazi wa hapa wanaangukia katika wizara yangu maana wao ni wavuvi, kwa maana hiyo nina jukumu kubwa la kuwasaidia, na hivyo natangaza kwamba serikali itajenga bweni moja ili wanafunzi waanze kuishi hapo shuleni,” alisema Waziri Mpina.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation Bi. Rosalynn Mworia aliunga mkono juhudi za serikali kwa kuahidi kwamba taasisi yake itanunua magodoro na vitanda kwa ajili ya bweni hilo pindi litakapokamilika.

“Tumefurahishwa sana na uamuzi wa serikali wa kujenga bweni hilo, maana hii itaokoa vipaji vingi ambavyo vingeweza kupotea aidha kwa kukata tamaa maana usafiri wa kwenda shule ni mgumu, au kutokea kwa majanga ya majini, hivyo basi pindi bweni hilo litakapokamilika sisi tutaleta vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi hao,” alisema Mworia.

Mwanafunzi Editha Fabian kutoka Bwiro Sekondari alisema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali maana utawafanya wasome kwa bidii zaidi, “tutakuwa katika mazingira salama, hatutachoka maana muda mwingi tutautumia kusoma badala ya kuwa safarini huku tukiwaza kuzama majini,” alisema Editha.

Waziri Mpina pia aliziomba taasisi zote mbili kuandaa mpango mkakati endelevu wa miaka mitatu ili kutoa elimu ya majanga kwa wakazi wa kanda ya Ziwa Victoria, “mkifanya hivi mtafikia watu wengi zaidi na pia kutakuwa na uendelevu wa juhudi zenu za pamoja, tafadhali kaeni chini miliangalie hili kwa kina zaidi,” aliongeza Waziri Mpina.

No comments:

Post a Comment