Dar es Salaam; October 25, 2018 - Benki ya biashara ya DCB imefanikiwa kupata faida ya shilingi bilioni 1.4 katika kipindi kinachoishia mwezi Septemba mwaka 2018 huku ikiipiku hasara ya shilingi bilioni 1.6 iliyopatikana kipindi kama hicho mwaka 2017 ambayo inawakilisha ongezeko la asilimia 187.
Benki imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha inatoka kwenye hasara iliyopata mwaka 2017 na kurudi kwenye faida. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa in kuboresha mfumo wa endeshaji biashara ambapo gharama za uendeshaji zimeshuka na huduma mpya za kidigitali zimeanzishwa ambapo zimevutia wateja wengi zaidi kufungua account na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama zitokanazo na amana za wateja.
Moja ya huduma za kidigitali ambazo benki imezindua ni akaunti ya kidijiti (DCB Digital Account), DCB Kibubu Digital Account, DCB FDR Digital account. Account hizi zinamuwezesha mteja kufungua akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, Kutunza pesa na kuwekeza kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Ukuaji wa faida umechagizwa na ukuaji wa mikopo ghafi ya wateja kutoka shilingi bilioni 89.3 mwezi Septemba, 2017 kufikia shilingi bilioni 91.3 mwezi Septemba, 2018. Ukuaji huu umechagizwa na utoaji wa mikopo ambapo mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 50 imetolewa hadi kufikia mwezi Septemba 2018. Idadi ya wateja imeongezeka kutoka 144,445 mwezi Desemba 2017, kufikia wateja 157,366 mwezi Septemba 2018.
Mapato halisiya benki yatokanayo na riba yameimarika katika robo ya tatu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita hali ambayo imechagizwa na mkazo wa benki katika kuongeza amana za gharama nafuu kupitia bidhaa za amana za kidijiti, usimamizi wa mizania wenye ufanisi na usimamizi wa gharama za uendeshaji wa benki. Uwiano wa mikopo ghafi na jumla ya amana za benki umeongezeka kwa asilimia 3.1 ikilinganishwa na robo ya pili ya mwaka huu.
Ili kuhakikisha ufanisi wa mizania, benki imeendelea kulinganisha amana aghali na zenye unafuu, ili kuendana na hali ya amana katika masoko ya kibenki ambapo amana za wateja zimepungua katika robo ya tatu ya mwaka 2018 ikilinganishwa kipindi kama hicho mwaka 2017. Upunguaji huu wa amana aghali umechangia kupungua kwa gharama za riba za amana na kuiwezesha benki kutoa mikopo nafuu kwa wateja, kuongeza mapato halisi na faida kwa ujumla.
Pamoja na ongezeko la mikopo ghafi, benki ya DCB imefanikiwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu kutoka asilimia 18.9 mwezi Desemba 2017 kufikia asilimia 17.8 mwezi Septemba 2018 (Juni 2018 asilimia 17.7). Upunguaji huu umechagizwa na ongezeko la ufanisi katika ukusanyaji wa madeni, utoaji wa mikopo kwa riba nafuu na kuboreshwa kwa huduma kwa waateja.
Benki ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa kama Benki ya Jumuiya ya Wananchi “community bank” na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kufuatia kilio cha wakazi wengi wa Jiji kutokuwa na njia rahisi ya kupata mitaji midogo midogo ya biashara. Katika miaka yake 16 ya utoaji huduma, benki imeongeza idadi ya wateja kufikia 157,366 mwezi Septemba mwaka 2018, idadi hii ni kubwa kwa sababu benki ya DCB inalenga zaidi wananchi wa kipato cha chini. Benki ya DCB ambayo ni ya kwanza kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa, imeweza kukuza mtandao wake wa matawi kufikia matawi nane likiwepo tawi la Dodoma, na inatarajia kuongeza matawi mengine mikoani katika miaka ya mbeleni.
Benki imjiimarisha zaidi katika teknohama na mifumo mbalimbali ya utoaji huduma huku ikiwa mstari wa mbele katika utoaji wa mitaji midogo kwa wananchi wa kipato cha chini, ambapo hadi mwishoni mwa mwezi wa Septemba 2018, imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi billioni 150 kwa wafanyabiashara wadogo wa vikundi, ikiwemo shilingi billioni 16 zilizotolewa kwa mfuko wa wanawake na vijana wa halmashauri za Jiji la Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment