Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 14 August 2018

MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA SADC WAFUNGULIWA MJINI WINDHOEK, NAMIBIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika unaofanyika tarehe 13 na 14 Agosti 2018 katika hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena L. Tax (mstari wa mbele kati) akiwa katika picha ya pamoja na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika mara baada ya hafla ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Windhoek, Namibia. 
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, Dkt. Stergomena L. Tax akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa SADC. Katika hotuba yake aliwasilisha taarifa fupi ya mwaka ya utekelezaji ya Jumuiya hiyo pamoja na kuishukuru Serikali ya Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda) kwa uongozi na usimamizi mzuri katika kipindi chote cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.
Mkutano ukiendelea. Walioketi nyuma ya Mhe. Waziri Mahiga kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Viwanda na Mawasiliano (anayeshughulikia masuala ya ujenzi) Mhandisi Joseph Nyamhanga. 
Mkutano ukiendelea. Kutoka Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Mhede.
Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Namibia mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini, Mhe. Sylivester Ambokile na wajumbe wengine wa Serikali ya Tanzania wakifuatilia ufunguzi wa mkutano.
Mkutano wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) umefunguliwa rasmi katika Hoteli ya Safari mjini Windhoek, Namibia tarehe 13 Agosti 2018.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ambaye ameambatana na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania ambao ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda; Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayesimamia masuala ya Ujenzi) Mhandisi Joseph Myamhanga, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu na Naibu Katibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Edwin Paul Mhede

Mkutano huu ni sehemu ya mikutano ya awali ya maandalizi ya mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 na 18 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia. Mikutano mingine ya awali ni mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika tarehe 9 na 11 Agosti 2018 na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa , Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018.

No comments:

Post a Comment