Foreign Exchange Rates

DStv Advert_010224

DStv Advert_010224

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 14 August 2018

ACTL WAJIPA MIAKA SITA KUPATA FAIDA

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linatarajia kuanza kupata faida mwaka 2023 endapo mpango wake wa kibiashara utatimia na mwenendo wa biashara ukiendelea kuimarika kama ilivyo sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Ladislaus Matindi alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi kutoa ufafanuzi wa kile alichozungumza meneja mauzo na usambazaji wa ATCL, Edward Nkwabi wakati wa mkutano na mawakala wa tiketi za shirika hilo.

Matindi alisema hivi sasa shirika linapambana kuhakikisha linapunguza hasara katika biashara kupitia mpango wa kibiashara wa mwaka 2017/2022.

Awali, meneja mauzo na usambazaji wa ATCL, Nkwabi akizungumza na mawakala wa tiketi za shirika hilo alisema limefanikiwa kuongeza mapato hadi kufikia Sh4.5 bilioni kwa mwezi mwaka 2017 tofauti na mwaka 2016 yalipokuwa Sh700 milioni kwa mwezi.
Nkwabi alisema kiwango cha hasara katika shirika hilo lililoanza kufufuliwa mwishoni mwa mwaka 2016 nacho kimepungua kutoka Sh14.2 bilioni mwaka huo hadi Sh4.3 bilioni mwaka 2017.

Akizungumzia mwenendo wa kifedha wa shirika hilo, mkurugenzi mtendaji Matindi alisema linajiendesha kwa hasara kutokana na madeni ambayo menejimenti mpya imeyakuta.

“Tuna mpango wa kibiashara wa miaka mitano mpaka 2022, endapo mwenendo wa biashara ukiendelea kama sasa mpaka 2023 tutakuwa tumesahau suala la loss (hasara),” alisema Matindi.

Alisema mpaka kufikia wakati huo, shirika litakuwa limejiimarisha kibiashara na hawatarajii kuwa na hasara zinazotokana na uzembe, ufisadi au usimamizi mbovu kama ilivyokuwa awali, labda iwe ni hasara ya kibiashara.

ATCL ambayo sasa ukubwa wake katika soko la ndani ni asilimia 24, iliwaeleza mawakala wa tiketi zake kuwa ina mpango wa kuimarisha kituo cha huduma kwa wateja.

Pia, itaongeza safari katika maeneo ya ndani na nje ikiwamo safari mpya za Entebe, Uganda na Bujumbura, Burundi mwezi huu.

Nkwabi alisema safari nyingine ni ya Mumbai, India inayotarajiwa kuanza Septemba na Guangzhou, China mwishoni mwa mwaka. “Tutaendelea kuongeza safari mpya nchini na nje ya nchi kama ilivyo katika mpango wetu wa kibiashara na hasa kuwa na ndege za moja kwa moja katika maeneo ambayo watalii wengi wanaokuja nchini wanatokea huko,” alisema Nkwabi.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya uwakala ya ABC Travel and Tours, Saleh Pamba alihoji ni kwa nini ATCL haisikiki ikipanga kuanzisha safari kati ya Ulaya na Amerika ambako asilimia 70 ya watalii wote wanaokuja nchini wanatokea huko.

Matindi akijibu swali hilo, alisema kwa sasa wanajiimarisha kwanza ili kuwa washindani katika maeneo hayo.

Alisema uwezo wao sasa ni kwenda India na China ambako kuna abiria wengi, lakini ushindani ni mdogo.

“Mpango wetu wa biashara unaonyesha baada ya ujio wa Dreamliner nyingine tutakuwa na safari ya London (Uingereza). Soko la Amerika na Ulaya ni kubwa kwa kuwa na idadi kubwa ya abiria lakini kuwapata si rahisi kutokana na ushindani uliopo. Tukishajiimarisha zaidi tutaweza kwenda huko,” alisema Matindi.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment