Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Monday, 20 August 2018
KONGAMANO LA TANO DIASPORA LAFANYIKA MJINI CHAKE CHAKE, KISIWANI PEMBA
Watanzania waishio ughaibuni wamekutana Chake Chake, kisiwani Pemba tarehe 18 na 19 Agosti, 2018 katika Kongamano la Tano la Diaspora kufuatia utaratibu uliowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwakutanisha kila mwaka Watanzania waishio ughaibuni.
Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya Idara ya Ushirikano wa Kimataifa na uratibu wa masuala ya Diaspora pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki liliwakutanisha Wanadiaspora zaidi ya 300 katika viwanja vya Tibirinzi, Pemba. Wadau mbalimbali wa hapa nchini kutoka Serikalini na Sekta binafsi walihudhuria Kongamano hilo.
Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa mgeni rasmi akiambatana viongozi wengne waliohudhuria kongamano walikuwepo; Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Haji Issa Ussi Gavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mawaziri, Makatibu na Manaibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Watendaji wa Serikali zote za Muungano.
Katika kongamano hilo Wanadiaspora hao walipata fursa ya kuwasilishiwa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Diaspora na Maendeleo; Uraia; Sheria za Uhamiaji na kufahamishwa fursa zilizopo nchini kwa ajili ya uwekezaji kwa manufaa Wanadiaspora na Taifa kwa ujumla. Aidha, Watanzania hao waishio ughaibuni walipata fursa ya kuuliza maswali pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu maswala mbalimbali yenye lengo la kuendeleza umoja huo na maendeleo ya Nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia Watanzania hao kuwa Serikali zao zinatambua umuhimu wa Watanzania waishio ughaibuni na hivyo itaendelea kuwashirikisha katika maswala mbalimbali ya maendeleo ya nchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais Shein aliwahimiza Wanadiaspora hao kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu na aliwasihi wazidi kuitangaza na kuwekeza nchini kwa wingi.
Nae mwakilishi wa Watanzania waishio ughaibuni Bw. Adolf Makaya, Katibu wa Baraza la Dunia la Diaspora (TGDC), kwa niaba ya wanadiaspora hao, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwathamini na kutambua umuhimu wao katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.
Sambamba na hayo, Wanadiaspora walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo kisiwani Pemba ikiwa ni pamoja na kutembelea hoteli ya kitali ya Manta Resort iliyopo Makangale kisiwani Pemba. Hoteli hiyo imekuwa gumzo na kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwa na chumba kilicho chini bahari.
Akifunga kongamano hilo, Balozo Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alifurahishwa na mahudhurio mazuri ya Wamadiaspora na kuona kuwa ni fursa kubwa kwao kuona maendeleo ya nchi yao na pia kujenga maelewano mazuri na Serikali.
Kwa ujumla, kongamano hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa ambapo viongozi wa Serikali pamoja na wanadiaspora hao waliweza kupata fursa ya kujadiliana namna mbalimbali za kiwashirikisha Wanadiaspora hao katika maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.
Imeandaliwa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
19.08.2018
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment