Miongoni mwa benki za kwanza kutekeleza sera ya fedha ya Benki Kuu
BancABC, ambayo ni sehemu ya Atlas Mara iliyosajiliwa katika Soko la Hisa la London imepiga hatua kwa mara nyingine katika soko nchini kwa kutangaza punguzo katika tozo za mikopo ili kutoa ahueni kwa wateja wake wakati wa ulipaji wa mikopo na kuwawezesha wateja wapya kukopa kuanzia Aprili 1, 2018.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa BancABC, Bw. Dana Botha alisema watapunguza riba kwenye mikopo ya masharti, huduma ya over draft, na mikopo ya nyumba kwa wateja wao.
“Mwaka jana benki nyingi zilipita katika wakati mgumu wa ukwasi, hivyo kufanya uwezo wa kukopesha kuwa mdogo. Kwa miezi kadhaa sasa, serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuhusu punguzo la riba hili kwa kusaidia kupunguza masharti kama vile kiwango cha chini cha fedha kwa mabenki, viwango vya punguzo, hati fungani za hazina na kukopesha mabenki kwa viwango vya chini. Hili limewezesha ukopeshaji kwa watu binafsi na makampuni mbalimbali ili kuimarisha biashara zao na hatimaye kuboresha uchumi na tunajivunia kuwa kati ya benki za kwanza kutangaza wazi kuhusu punguzo hili,” alisema.
Alisema wateja wa BancABC watanufaika kwa kulipa mikopo yao kwa viwango vya chini zaidi vya marejesho ya awali au kupata mkopo mpya kwa riba nafuu. “Tuna imani kuwa baada ta taarifa hii, wateja wengi zaidi sasa watabisha hodi BancABC,” alisema na kuongeza kuwa hatua hii itawavutia watu binafsi na wafanyabiashara mbalimbali katika miji na vijiji ili waboreshe maisha yao na biashara zao na kukuza uchumi.
“Viwango vikubwa katika tozo za mikopo imekuwa changamoto kwa watanzania wengi hasa wale wa daraja la kati na la chini lakini sasa tunaamini kuwa hata wale ambao hawakuweza kukopa sasa watatumia fursa hii kuboresha biashara zao na maisha yao kwa ujumla,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Dana, hatua hizi mpya za serikali zitachochea ukuaji wa uchumi na benki nyingi zitaweza kukopesha na sio kuwekeza katika hati fungani za hazina na serikali, hili litachochea wateja kukopa zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha wateja binafsi na Wafanyabiashara wa BancABC, Joyce Malai alisema BancABC inahudumia zaidi ya wateja 60,000 ambao wanamiliki bidhaa tofauti za Kibenki, hivyo hii fursa itawawezesha kuwashawishi wateja wao kupata bidhaa zaidi ya moja hasa mikopo ya nyumba ambayo ilikuwa changamoto kubwa hasa kwa wananchi wa daraja la kati na chini. Tutatumia fursa hii pia kuimarisha wafanya biashara wetu wote na makampuni mbalimbali kupata mikopo nafuu na huduma ya overdraft kutoka moja ya shirika bora la kifedha nchini.
“Taarifa hii ya leo ni hatua kubwa sana kwa BancABC huku ikitazamia kuwa moja ya benki bora kusini mwa jangwa la Sahara na kulenga kuwa kati ya tano bora katika nchi tunazofanya kazi,” alisema Malai na kuongeza kuwa BancABC inaongoza katika juhudi hizi za Benki Kuu ya Tanzania za kupunguza viwango vya tozo za ukopeshaji.
KUHUSU ABC HOLDINGS
ABC Holdings ni kampuni mama ya benki kadhaa katika ukanda kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zinafanya kazi kwa jina la BancABC, ambayo inatoa huduma mbalimbali za kifedha.
KUHUSU ATLAS MARA
Atlas Mara iliorodheshwa katika soko la hisa la London Disemba 2013. Atlas Mara ina lengo la kujitanua na kuwa kinara katika masuala ya kifedha katika ukanda wa Sahara kwa kutumia uzoefu wake na uwezo wa kukuza mitaji. Malengo yake ni kuunganisha na kukuza uwezo wa taasisi za kifedha na pia kuendeleza uchumi katika nchi ambazo inafanya shughuli zake.
Mwaka 2014, Atlas Mara ilinunua hisa nyingi za ABC Holdings. Huku ikiongozwa na weledi wa hali ya juu pia ikijiwekea mazingira ya kuwa benki bora kabisa Afrika kwa kutoa huduma bora kwa wateja wake.
No comments:
Post a Comment