Dar es Salaam Tanzania, Septemba
25, 2017 – Benki ya CRDB leo imekabidhi
msaada wa shilingi milioni 100 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa
Paul Makonda, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi za walimu kwa shule za
msingi na sekondari mkoani humo. Msaada huo ni muendelezo wa utekelezaji wa
sera ya kusaidia jamii ya Benki ya CRDB inayoelekeza kutenga asilimia moja ya
faida yake kila mwaka ili zitumike katika shughuli za kijamii kwenye maeneo ya
afya, elimu na mazingira.
Akizungumza kabla
ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles
Kimei alisema Benki hiyo inatambua kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa
letu japo kuna changamoto nyingi zinazoikabili. “Tunatambua kuwa ili taifa letu
liweze kupiga hatua za kimaendeleo, ni lazima tuungane kwa pamoja na kuwekeza
katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kuweka
mazingira bora ya ufundishaji na ufundishwaji, jambo ambalo litaboresha viwango
vya elimu yetu na kuleta matokeo chanya” alisema Dokta Kimei.
“Tunajivunia
kuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya elimu nchini ambapo kwa mwaka huu 2017
pekee, tayari Benki ya CRDB imeshatumia zaidi ya shilingi milioni mia tatu
katika kufadhili ujenzi wa majengo ya madarasa katika shule mbalimbali nchini,
ikiwamo shule za msingi Msasani na Uhuru Mchanganyiko zilizopo mkoa wa Dar es
Salaam, shule za msingi Boma na Usa-River zilizopo mkoa wa Arusha pamoja na
shule ya msingi Ruangwa iliyopo Lindi pamoja na” alisema Dokta Kimei.
Akizungumza kuhusu msaada huo wa shilingi milioni
mia moja, Dokta Kimei alisema kuwa
anaamini msaada huo utafanikisha ununuzi wa jumla ya mifuko 10,000 ya saruji ambayo itasaidia kujenga jumla ya vyumba
vya ofisi za walimu 40 katika mkoa wa
Dar es Salaam. “Kifupi ni kuwa benki ya CRDB, leo inajitolea kujenga majengo 40
ya ofisi za walimu wa mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Dkt. Kimei.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa
Benki ya kizalendo yenye kujali mahitaji halisi ya wananchi.
“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam,
napenda kuishukuru kwa dhati kabisa Benki ya CRDB kwa msaada huu mkubwa na kwa
kuendelea kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine hapa nchini. Msaada huu wa
shilingi milioni 100 waliotupa leo, unatusogeza karibu zaidi na ndoto yetu ya
kujenga ofisi nyingi za walimu mkoani kwetu ili kujenga mazingira bora ya kazi
kwa walimu wetu na hivyo kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa
watoto wetu” alisema Mkuu wa Mkoa.
Akizungumzia hali ilivyo hivi sasa, Mheshimiwa
Makonda alisema “Sote tunajua ni jinsi gani walimu wamekuwa wakikosa motisha ya
ufanyaji kazi kutokana na mazingira magumu wanayokumbana nayo. Msaada huu
unatupa faraja kubwa sana ya kuwa zipo taasisi za kizalendo kama Benki ya CRDB zinazoguswa
na changamoto zinazotukabili. Naomba nikuhakikishie Dokta Kimei ya kuwa msaada
huu utaenda kufanya kazi iliyokusudiwa”.
Mheshimiwa Makonda
pia aliwasihi wadau wengine kuendelea kuchangia zoezi hilo kupitia akaunti
maalum ya uchangiaji wa ujenzi wa ofisi hizo yenye nambari “0150296180200” iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe jijini
Dar es Salaam.
Maelezo jinsi ya kuchangia Ujenzi Ofisi
za walimu Jijini Dar es Salaam:
Michango yote itumwe kwenye akaunti nambari
iliyopo katika “0150296180200” iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe
jijini Dar es Salaam.
Njia za kuchangia:
- Kupitia tawi lolote la Benki ya CRDB lililo karibu naw
- Kupitia Huduma ya SimBanking kwa kupiga *150*03# na kisha kufuata maelekezo ya kuhamisha fedha
- Kupitia Mawakala wote wa FahariHuduma wa Benki ya CRDB waliopo chi nzima
- Kupitia kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti za mitandao yasimu na kupeleka kwenye akaunti 0150296180200 ya Benki ya CRDB
Kwa maelezo
zaidi, tafadhali wasiliana na:
Jina
|
Namba ya Simu
|
Barua Pepe
|
Tully Esther Mwambapa
|
+255 769 200 600
|
|
Godwin Semunyu
|
+254 784 002020
|
No comments:
Post a Comment