Mwanasheria toka Baraza
la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Manchare Heche akionesha kwa
waandishi wa habari moja ya pombe kali aina ya Nguvu zilizokamatwa wakati wa
operesheni inayoendelea mapema leo hii jijini Dar es Salaam wakati wa siku ya
nne ya operesheni ya kusaka wasambazaji wa kinywaji hicho ambacho Serikali
imepiga marufuku kutumika.
Msimamizi wa ghala la Love kira Enterprises
lililopo Wazo Bi. Sia Mboya (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mwanasheria toka
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Manchare Heche (katikati)
wakati wa operesheni ya kuondoa pombe hiyo katika soko, kulia ni Afisa Afya
toka Manispaa ya Kinondoni Bw. John Kijumbe.
Gari lililokutwa limebeba pombe kali aina ya kiroba original likiwa limeegeshwa nje ya duka la kuuzwa vinywaji la Love Kira lililopo Wazo jijini Dar es salaam mapema leo.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika msako wa pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01 mpaka 03, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali ya kusitisha pombe hizo za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
“Jumla ya katoni 99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba) zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa na mililita 50, katoni 29,344 zenye ujazo wa mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa zenye ujazo wa mililita 100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,” alifafanua Makamba.
Aliendelea kwa kusema kuwa, jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala 4, baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika opesheni hiyo.
Makamba amesema kuwa, pombe zilizokamatwa zimezuiliwa kuuzwa au kusambazwa kutoka katika maeneo ambayo yamehifadhiwa yaani viwanda, maghala pamoja na maduka ya jumla mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko.
Aidha wananchi wametakiwa kushiriki katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kubaini wanaokaidi agizo la Serikali la kuzalisha, kusambaza, kuuza au kutumia pombe hizo kupitia namba ya simu 0685 333 444 kwa kutuma ujumbe mfupi wa meseji au whatsapp au kwa kupiga simu.
Vile vile amesema kuwa zawadi kati ya shilingi laki 5 hadi milioni 1 zitatolewa kwa mwananchi atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha sheria, watu au mtu anayeingiza pombe za viroba nchini kutoka nje ya nchi kinyume na sheria na utaratibu, anayehamisha au kusafirisha pombe za viroba kinyume na sheria, mtu mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha pombe za viroba ambao hautambuliki na Serikali pamoja na mtu anayetumia stempu feki za TRA .
Pombe za viroba zimechangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa, ajali na vifo vinavyosabaishwa na unywaji uliokithiri wa pombe hizo, kuongezeka kwa vitendo vyauhalifu na kupotea kwa mapato yanayosababishwa na wafanyabiashara wasio waamini.
Kutokana na athari hizo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa Mkoani Manyara, Februari 16 mwaka huu alitoa tamko la kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa pombe kali za viroba kwa nchi nzima kuanzia Marchi 01, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment