Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB nchini Tanzania, Bi. Ineke Bussemaker akiwa na mwenyeji wake Dk. Shein katika Ikulu ya Zanzibar hivi karibuni. |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa azma ya Benki ya NMB ya kuendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika jamii itasaidia kuimarisha uchumi na kuleta tija kwa wananchi wa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB nchini Tanzania Bi Ineke Bussemaker alipofika Ikulu mjini Zanzibar. Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Benki ya NMB imekuwa na mchango mkubwa katika kuzisaidia sekta za maendeleo hapa nchini zikiwemo sekta ya afya, elimu na nyinginezo hatua ambayo ni muhimu katika kufikia malengo yaliyokusudiwa
Aidha, Dk. Shein aliipongeza Benki hiyo kwa kuanzisha programu mbali mbali za kuwasaidia wakulima wakiwemo wa zao la karafuu hapa nchini na kueleza lengo la Serikali ni kuona zao la karafuu linaimarika na ndio maana imekuwa ikichukua juhudi za makusudi ili kuhakikisha zao hilo linapata sifa kimataifa. Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kuimarisha sekta za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NMB Tanzania, Bi Ineke Bussemaker alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika jamii na kuahidi kuendelea kuunga mkono.
“Benki ya NMB imeweza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi kadhaa ikiwemo miradi ya elimu kwa kusaidia madawati, afya, kilimo na tunaahidi kuendeleza miradi hii kwa lengo la kuinua kipato cha mwananchi wa Zanzibar. Pia tunaendelea na azma yetu ya kusaidia kompyuta 50 kwa skuli za Zanzibar ” aliongeza Bi Bussemaker
Pia, Mkurugenzi huyo alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Benki yake katika mradi wa kuwasaidia wakulima katika kuimarisha na kusafirisha bidhaa zao zikiwemo bidhaa za viungo na kusisitiza umuhimu wa kukusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kisasa wa “e-tax” ambapo benki yake tayari imeshaanza mchakato huo kwa upande wa Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment