Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday 21 July 2016

WAZIRI MAHIGA ASAINI MKATABA WA UENYEJI WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA MASHARIKI (EADB)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bi. Vivienne Yeda wakisaini Mkataba wa Uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za Benki hiyo nchini. Hafla hiyo ilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki tarehe 20 Julai, 2016.
Waziri Mahiga na Bi. Yeda wakibadilishana Mkataba mara baada ya kuusaini. 
Dkt. Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Bi. Yeda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Baraka Luvanda (kulia) na Mkuu wa Biashara wa EADB hapa nchini Bi. Juliana Sweke (kushoto). (Picha na Reginald Philip).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amesaini Mkataba wa uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bi. Vivienne Yeda. Mkataba huo umesainiwa jana katika Ofisi za Wizara kwa lengo la kurasimisha kisheria Ofisi za Benki hiyo zilizopo nchini.

Aidha, uwekaji saini wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 2 Machi, 2016 Mjini Arusha, Tanzania. Mkutano huo pamoja na mambo mengine uliazimia kuanzishwa kwa Ofisi za Benki hiyo katika Makao Makuu ya kila nchi Mwanachama ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa shughuli za Benki hiyo.

Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ni Taasisi ya Fedha iliyoanzishwa mwaka 1967 chini ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kutoa misaada ya kifedha na misaada mingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

EADB ilianzishwa wakati iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na wanachama watatu ambao ni Tanzania, Kenya na Uganda. Rwanda ilijiunga na Benki hiyo mwaka 2007 na kufanya nchi wananchama waliojiunga kufikia wanne.

Kwa upande wa Tanzania, EADB imeisaidia kutoa mikopo mbalimbali katika miradi ya maendeleo kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB). Pia, katika kulipa kipaumbele suala la Afya, Benki hiyo imeweka mpango wa kusaidia afya ya uzazi kwa akinamama hususan, katika maeneo ya vijijini.

Miradi mingine inayofadhiliwa na EADB hapa nchini ni pamoja na miradi ya Umeme hasa kwa maeneo ya vijijini, na miradi ya maji na usafi wa mazingira.

Akiongea katika hafla hiyo, Mhe. Waziri Mahiga aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha uendeshaji wa Benki hiyo unafanikiwa. “Karibuni sana na pale inapotokea mmekwama katika jambo lolote linalohitaji usaidizi wa Serikali au ushauri tupo tayari kutoa ushirikiano” alisema Waziri Mahiga.

No comments:

Post a Comment