Mtwara, Novemba 14, 2015: Ikiwa ni sehemu ya kusherekea maadhimisho ya siku ya Ecobank ambapo wafanyakazi wa benki hii barani Afrika huhamasishwa kujitolea muda wao kwa ajili ya shughuli za kijamii zenye manufaa kwa jamii husika,
Ecobank Tanzania ilisherekea siku hii kwa kukarabati moja ya wodi ya watoto katika hospitali ya Rufaa ya Ligula mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika mkoani Mtwara katika hospitali ya rufaa Ligula, Mkurugenzi mtendaji wa Ecobank Tanzania, Bw. Enoch Osei-Safo alisema benki yake imekuwa ikisherekea “Siku ya ecobank” nchini Tanzania kwa takribani zaidi ya miaka mitatu sasa na kuwa ni mpango unaolenga kusherekea na kuthamini jamii inayoizunguka Ecobank.
“Tunatambua taifa la kesho lipo mikononi mwa watoto wetu. Kwa kuhakikisha tunawapatia afya bora, watoto watakua wenye nguvu na ushupavu tayari kwa kukabiliana na Dunia”.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kila Mtoto wa Afrika anastahili maisha bora ya baadaye”
“Tungependa kusherekea na watoto wa Mtwara kwa kuwaboreshea mazingira katika wodi yao hapa hospitali ya rufaa ya Ligula. Tumejitolea muda wetu na rasilimali zetu kuweka mazingira safi na salama kwa ajili ya watoa huduma pamoja na watoto”.
Bw. Enoch Osei-Safo aliongezea kuwa sera ya uwajibikaji kwa jamii ya Ecobank Tanzania inawaongoza kutoa ushirikiano kwa jamii mbalimbali katika sekta kadhaa ikiwemo ya afya na elimu huku afya ikichukua asilimia 60 ya miradi yote ya uwajibikaji kila mwaka.
Akiwasilisha hotuba yake, Kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mtwara mjini, Bi. Fatma Ally aliyekuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo aliwapongeza Ecobank Tanzania kwa moyo wao mkunjufu katika kukarabati wodi ya watoto na kujitolea muda wao kukaa na watoto hao waliokuwa wamelazwa wodini hapo.
Bi. Fatma aliihimiza benki hiyo kupanua wigo wa uhisani wao katika sekta ya Elimu, Mazingira, Kilimo na masuala mengine yanayokabili jamii moja kwa moja na akawahakikishia kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za afya katika hospitali mbalimbali, elimu na mazingira mkoa mzima.
“Tumedhamiria kuendelea kufanya kazi na sekta binafsi pamoja na zile za umma ili kuhakikisha tunaboresha maisha ya mtoto wa Afrika”.
Naye Kaimu Mganga mkuu wa hospitali hiyo Bw. Joseph Mweru aliipongeza benki hiyo kwa mchango wao na kusema ukarabati huo utasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga ambao hupoteza maisha yao kwa kukosa mazingira safi, salama na hewa safi.
Takwimu zinaonyesha vifo vya watoto mkoani Mtwara mwaka 2014 vilifikia 385 kutoka 240 vya mwaka 2013. Sababu kwabwa ya ongezeko hili ni ukosefu wa hewa safi, malaria kali na maambukizo ya magonjwa mengine.
No comments:
Post a Comment