- Asisitiza siku za kuunganisha umeme kupungua
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kuipa vipaumbele vya utekelezaji wa majukumu vitakavyotekelezwa na Bodi hiyo kabla ya kufikia ukomo wake mnamo mwaka 2017.

Wajumbe wa Bodi ya TANESCO wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Mighanda J. Manyahi (wa sita kutoka kushoto) wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eng.Ngosi Mwihava (wa tano kulia) mara baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) kuizindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.Wajumbe wengine wa Bodi hiyo (kutoka kushoto) ni Dkt. Nyamajeje C. Weggoro, Eng. Boniface C. Muhegi, Dkt. Mutesigwa I. Maingu, Bw. Shaaban S. Kayungilo, na Dkt. Haji H. Semboja. Wajumbe wengine (kutoka kulia) ni Bibi. Kissa Vivian Kilindu, Bw. Felix G. Kibodya na Eng. Juma F. Mkobya.
Uzinduzi wa Bodi hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini na kuhudhuriwa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini akiwemo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Ngosi Mwihava na Menejimenti ya Tanesco.
Waziri Muhongo aliieleza Bodi hiyo kuwa ina jukumu kubwa la kuliongoza Shirika hilo kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa Shirika hilo linajitegemea na hivyo kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.
“Kwa kipindi kirefu, serikali imekuwa inatoa fedha nyingi kuisaidia Tanesco kutekeleza miradi katika maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme hivyo Bodi hii ionyeshe jinsi mtakavyolibadilisha Shirika hili ili hii misaada kutoka serikalini ipungue na ifike mahala Shirika hili lijitegemee,” alisema Profesa Muhongo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kutoka kushoto), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele (wa tatu kutoka kushoto), Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eng.Ngosi Mwihava (wa nne kutoka kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Eng. Felchesmi Mramba (wa pili kulia), wakimsikiliza mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO (haonekani pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo, Eng. Juma Mkobya.
Suala la wananchi kufungiwa umeme ndani ya siku 30 mara wanapopeleka maombi hayo Tanesco lilimkera Profesa Muhongo na kuiagiza Bodi hiyo kulishughulikia suala hilo ili siku hizo zipungue.
“Bodi simamieni maombi ya kufungiwa umeme ambayo sasa yanaelezwa kushughulikiwa ndani ya siku 30, hii lazima ibadilike, watanzania lazima wapewe umeme ndani ya wiki, zaidi ya hapo haikubaliki. EWURA waelezwe kuhusu suala hili ili kuona namna ya kupunguza hizi siku sababu wao wanahusika katika suala la upangaji wa siku husika,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Mighanda J. Manyahi (aliyesimama) akizungumza mara baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuizindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam. Wanaomsikiliza ni Waziri, Profesa Muhongo (kulia) na Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt. Haji H. Semboja (kushoto).
Vilevile Profesa Muhongo aliiagiza Bodi mpya ya Tanesco kuhakikisha kuwa Shirika hilo linashirikiana na sekta binafsi katika miradi yake ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ili kufanikisha lengo la serikali la kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Profesa Muhongo alieleza kuwa kulingana na sera zilizopo, uendelezaji wa sekta ya umeme unahitaji ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa kuwa uwekezaji katika sekta hiyo unahitaji kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, kiwango ambacho kinahitaji ushirikiano na sekta hizo kupitia mitindo ya IPP na PPP. Alisema Tanesco inapaswa kuonesha nia thabiti ya kuunga mkono juhudi za serikali za kukamilisha majadiliano na wawekezaji na waendelezaji wa miradi bila kuwakatisha tamaa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Mighanda Manyahi ameeleza kuwa majukumu waliyokabidhiwa ya kuisimamia Tanesco ni makubwa lakini kwa kutumia taaluma zao watahakikisha wanayatimiza ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa kuwa nchi zina rasilimali za kutosha zinazowezesha kutimiza lengo hilo.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco anaongoza wajumbe Nane ambao ni Bibi. Kissa Vivian Kilindu, Mhandisi Juma Mkobya, Dkt. Haji H. Semboja, Bw. Shaaban Kayungilo, Dkt. Mutesigwa Maingu, Mhandisi Boniface Muhegi, Bw. Felix Kibodya, na Dkt. Nyamajeje Weggoro.
Imeandaliwa na:
Teresia Mhagama,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
754/33 Mtaa wa Samora,
S.L.P 2000 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606
Barua Pepe: info@mem.go.tz
Tovuti: mem.go.tz
No comments:
Post a Comment