Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Friday, 6 February 2026

VODACOM TANZANIA FOUNDATION YAWEKA KAMBI ZA AFYA BURE KARIBU NA JAMII YA ZANZIBAR

Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani (wapili kushoto), akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya huduma za afya iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania Foundation. Kambi hiyo inalenga kutoa huduma za bure za upimaji wa afya, ushauri na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.

Tukio hilo lilifanyika Visiwani Zanzibar na kushuhudiwa na Kaimu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi (kushoto), pamoja na Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald (wapili kulia).

Zanzibar, Februari 4, 2026 – Nchini Tanzania, magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanaendelea kuwa changamoto kubwa kwa afya ya jamii, yakichangia takribani asilimia 34 ya magonjwa sugu yote. Magonjwa kama shinikizo la damu na kisukari mara nyingi hugundulika yakiwa tayari katika hatua za juu, hasa katika jamii zenye ufinyu wa huduma za uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, hali inayoongeza hatari ya madhara ya muda mrefu kiafya.

Hali hiyo pia inaonekana Zanzibar, ambapo wataalamu wa afya wamekuwa wakibainisha ongezeko la wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari. Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuimarisha juhudi za kinga, uchunguzi wa mapema pamoja na elimu ya afya kwa jamii ili kupunguza athari za magonjwa hayo.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Vodacom Tanzania Foundation inaendelea kutekeleza mpango wake wa muda mrefu wa kambi za afya bure, ambao umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa saba na wilaya 16 nchini. Mwaka huu, mpango huo umeanza kutekelezwa Zanzibar kwa mara ya kwanza, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Foundation ya kupanua wigo wa huduma za afya za kinga kwa jamii mbalimbali.

Kambi hiyo ya afya, inayofanyika kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026, inalenga uchunguzi wa mapema na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kupitia huduma za upimaji wa afya, ushauri wa kitaalamu pamoja na elimu ya afya kwa wananchi.

Umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuboresha afya ya jamii ulidhihirishwa wakati wa ufunguzi rasmi wa kambi hiyo uliofanyika Jumatano, Februari 4, 2026, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Marijani alisisitiza mchango wa mipango ya kinga katika kupunguza athari za muda mrefu za magonjwa yasiyoambukiza.

“Shinikizo la damu na kisukari vinaendelea kuwaathiri wananchi wengi Zanzibar, mara nyingi bila dalili za awali. Mipango inayohamasisha uchunguzi wa mapema, uelewa na hatua za kinga ni muhimu katika kusaidia jamii kudhibiti magonjwa haya na kuzuia madhara makubwa kiafya,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, alisema kambi hizo zimebuniwa mahsusi kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

“Mpango huu unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma na kuleta athari chanya kwa jamii. Kwa kupeleka huduma za afya za kinga moja kwa moja kwa wananchi, tunawawezesha kuchukua hatua mapema kuhusu afya zao. Kuanza Zanzibar mwaka huu ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa mpango huu,”alisema Sandra.

Aliongeza kuwa Vodacom Tanzania Foundation itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya na wadau mbalimbali ili kupanua mpango huo katika maeneo mengine, ikijenga juu ya uzoefu na mafanikio ya miaka iliyopita.

Mpango huu ni sehemu ya mchango mpana wa Vodacom Tanzania Foundation katika kuunga mkono Lengo la Maendeleo Endelevu namba 3 (SDG 3): Afya Njema na Ustawi, linalolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote.

Foundation hiyo imewahimiza wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hiyo ya afya, ikisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema, uelewa na kinga ni nguzo muhimu katika kujenga familia zenye afya njema na jamii imara.


No comments:

Post a Comment