Dar es Salaam, Februari 5, 2026 – Pombe haramu zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wananchi, mapato ya Serikali na ustawi wa biashara halali nchini Tanzania, kwa mujibu wa utafiti mpya uliochapishwa.
Utafiti huo umebaini kuwa takribani asilimia 61 ya pombe zote zinazotumiwa nchini ni haramu, hali inayosababisha Serikali kupoteza karibu shilingi trilioni 1.026 kila mwaka kutokana na mapato ya kodi yasiyokusanywa.
Tanzania Yaungana na Mwelekeo wa Kikanda
Matokeo ya utafiti huo yanaakisi mwenendo unaoonekana pia katika nchi jirani. Tafiti zilizofanywa na Euromonitor International nchini Kenya na Uganda mwaka 2025 zilionesha kuwa pombe haramu zilichangia asilimia 60 na 67 ya matumizi ya pombe katika nchi hizo, mtawalia.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii inaonesha kuwa tatizo la pombe haramu si la kitaifa pekee, bali ni changamoto ya kikanda inayohitaji mbinu za pamoja na za muda mrefu.
Pombe Haramu Ni Nini?
Utafiti unafafanua pombe haramu kama vinywaji ambavyo havikidhi matakwa ya kodi, udhibiti na sheria. Hii inajumuisha pombe:
- Zisizolipiwa ushuru stahiki
- Zisizo na vibali vya afya
- Zinazokiuka viwango vya uzalishaji
- Zinazotumia viambato visivyoidhinishwa
Aidha, pombe haramu husambazwa kupitia vituo visivyo na leseni, ambavyo hasa katika nchi zinazoendelea vina mchango mkubwa katika soko la pombe.
Pombe za Kienyeji Zatawala Soko la Pombe Haramu
Utafiti unaonesha kuwa pombe haramu zimeenea katika makundi yote, ikiwemo pombe kali, bia na divai. Hata hivyo, mchango mkubwa unatokana na pombe za kienyeji zisizo halali au za asili kama vile Mbege, Komoni, Wanzuki, Ulanzi, Dengerua, na nyinginezo.
Ingawa pombe hizi zina nafasi ya kiutamaduni, matumizi yake kwa kiwango kikubwa yanachochewa na gharama nafuu. Kwa mfano, gongo, ambayo imepigwa marufuku, inaweza kuwa hadi asilimia 80 nafuu zaidi ikilinganishwa na pombe kali halali. Pombe bandia na zile zinazoingizwa kwa njia za magendo nazo zinaendelea kuwa changamoto, hususan katika makundi ya pombe kali na bia.
Hatari Kubwa kwa Afya ya Wananchi
Mbali na hasara za kiuchumi, pombe haramu zinaweka afya za walaji katika hatari kubwa. Uzalishaji usiozingatia viwango vya usalama na uwezekano wa matumizi ya kemikali hatarishi huongeza hatari za magonjwa, ulemavu na vifo.
Hatari hizi zimeendelea kuongezeka kadri soko la pombe haramu linavyokua kwa kasi zaidi kuliko soko la pombe halali.
Serikali Yataka Hatua za Haraka
Akizungumza wakati wa kutolewa kwa matokeo ya utafiti huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dennis Londo, alisema takwimu hizo zinaonesha changamoto inayohitaji hatua za haraka na za pamoja.
“Kupotea kwa zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka kutokana na pombe haramu kunapunguza uwezo wa Serikali kugharamia huduma muhimu za kijamii na kulinda afya za wananchi. Utafiti huu unatupa ushahidi muhimu wa kusaidia maamuzi ya sera na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau,” alisema.
Gongo Yachangia Hasara Kubwa Zaidi
Kwa mujibu wa utafiti huo, pombe za kienyeji zisizo halali, maarufu kama gongo, pekee zinachangia hasara ya takribani shilingi bilioni 709 kwa mwaka. Hasara nyingine zinatokana na pombe bandia, pombe za magendo, pamoja na ukwepaji wa kodi kupitia ulipaji pungufu au kuepuka kabisa ushuru.
Kwa Nini Utafiti Ulifanyika?
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga, alisema ukosefu wa takwimu za kuaminika ulikuwa kichocheo kikuu cha kuagiza kufanyika kwa utafiti huo.
“Bila takwimu sahihi, inakuwa vigumu kubuni hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili. Utafiti huu umefanywa ili kuonesha ukubwa halisi wa tatizo na kusaidia maamuzi yanayozingatia ushahidi,” alisema.
Kwa upande wake, mshauri wa Euromonitor International, Benjamin Rideout, alisema walitumia mbinu mseto, ikiwemo kutembelea maeneo yanayouza pombe haramu, kufanya mahojiano na wadau pamoja na tafiti kwa walaji, ili kupata picha halisi ya soko.
Sekta Binafsi Yaunga Mkono Juhudi
Kwa upande wa sekta binafsi, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ilisema ushirikiano wake na CTI unatokana na wajibu wa kulinda walaji na kuimarisha ushindani wa haki.
“Pombe haramu zinahatarisha maisha ya walaji, zinapunguza mapato ya Serikali na kudhoofisha biashara zinazofuata sheria. Ushiriki wetu ni mchango wa kupata suluhisho la kudumu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Obinna Anyalebechi.
Mapendekezo ya Utafiti
Utafiti unapendekeza hatua kadhaa muhimu, ikiwemo:
- Kuimarisha udhibiti wa ethanol
- Kuongeza ulinzi wa mipaka na udhibiti wa ndani
- Kuimarisha elimu kwa walaji kuhusu hatari za pombe haramu
- Kupanua matumizi ya teknolojia, ikiwemo mifumo ya uhakiki wa stempu za kodi
Hatua hizo zinatajwa kuwa muhimu katika kupunguza biashara ya pombe haramu na kulinda afya, mapato ya Serikali na mazingira ya biashara nchini Tanzania.


.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment