Manyara — Benki ya NMB imekabidhi vifaa mbalimbali vya elimu na afya vyenye thamani ya Shilingi milioni 105 kwa shule za msingi na sekondari pamoja na hospitali na zahanati katika Mkoa wa Manyara, ikiwa ni sehemu ya mchango wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana Wilayani Hanang, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Ladislaus Baraka, alisema msaada huo unalenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni, pamoja na kuinua ubora wa huduma za afya kwa wananchi.
Alibainisha kuwa vifaa vilivyotolewa vinawanufaisha shule na hospitali katika Wilaya za Hanang, Mbulu na Babati.
Msaada kwa Wilaya ya Hanang
Kwa Wilaya ya Hanang, NMB imekabidhi:
- Madawati 50 kwa Shule ya Msingi Gidamambula
- Vitanda 40 vya bweni (double decker) kwa Shule ya Sekondari Katesh
- Mabenchi 20 ya kupumzikia wagonjwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini)
- Mabati 200 kwa Shule ya Msingi Nanyemi
- Mabati 200 kwa Shule ya Msingi Mulbadaw
- Mabati 200 kwa Shule ya Msingi Ng’abati
Thamani ya vifaa hivi ni Sh Milioni 45, alisema Ladslaus.
Msaada kwa Wilaya ya Mbulu
Katika Wilaya ya Mbulu, benki hiyo imekabidhi:
- Viti 50 na meza 50 kwa Shule ya Sekondari Kainam
- Madawati 50 kwa Shule ya Msingi Kandach
- Viti 50 na meza 50 kwa Shule ya Sekondari Malang
- Madawati 50 kwa Shule ya Msingi Sambaray
- Meza 10 na viti 10 kwa walimu wa Shule ya Msingi Giting
- Vitanda viwili vya kujifungulia kwa wanawake wajawazito, vitanda 10 na magodoro 10 kwa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu
Vifaa hivi vimegharimu Sh Milioni 22.
Msaada kwa Wilaya ya Babati
Kwa Wilaya ya Babati, NMB imekabidhi:
- Madawati 50 kwa Shule ya Msingi Kiongozi
- Mabati 305 kwa Shule za Msingi Soraa na Singi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa
- Vifaa mbalimbali vya kuboresha huduma za afya katika zahanati mbili
Thamani ya msaada huo kwa Babati ni Sh Milioni 38.
Viongozi na Wananchi Waipongeza NMB
Wakuu wa Wilaya za Hanang, Mbulu na Babati waliipongeza Benki ya NMB kwa mchango wake unaogusa moja kwa moja mahitaji ya jamii, hususan katika sekta za elimu na afya.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Alimish Hazali, alisema msaada huo utasaidia kupunguza uhaba wa madawati katika shule za msingi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simindu, alisema wataendelea kuiunga mkono NMB kutokana na jitihada zake za kuendeleza huduma za kijamii katika mkoa huo.
Naye mwanafunzi Monica Allen wa Shule ya Msingi Sambaray, kwa niaba ya wanafunzi wengine, aliishukuru NMB kwa kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati, hatua ambayo itachangia kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni.
Msaada huu unaendeleza dhamira ya NMB ya kushirikiana na jamii na Serikali katika kujenga maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika elimu na afya.


.jpeg)


No comments:
Post a Comment