Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Thursday, 16 October 2025

NMB YAWEZESHA WAFANYABIASHARA 28 KUJIFUNZA MASOKO YA KIMATAIFA NCHINI CHINA

Dar es Salaam, Oktoba 2025 – Benki ya NMB imefadhili ziara ya kibiashara ya wafanyabiashara 28 wa Kitanzania kwenda China, yenye lengo la kuwapa uzoefu wa moja kwa moja wa masoko ya kimataifa na kuwaonesha fursa za kibiashara na uwekezaji katika nchi hiyo.

Ziara hii ni sehemu ya jitihada endelevu za benki hiyo katika kuwawezesha wateja wake kuboresha ushindani wao kwenye soko la dunia, kupata maarifa mapya kuhusu mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, mbinu bora za upatikanaji wa bidhaa, na kujenga ushirikiano wa kimkakati na wawekezaji wa China.

Katika kuhakikisha ufanisi wa programu hiyo, washiriki watatembelea viwanda, vituo vya biashara, pamoja na taasisi za Serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuibua fursa mpya za ushirikiano na maendeleo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw. Filbert Mponzi, alisema kuwa ziara hiyo ya siku tisa itaanza leo na itahusisha ushiriki wa washiriki katika Maonyesho ya 138 ya Biashara ya Kimataifa ya Canton, mojawapo ya maonesho makubwa zaidi duniani.

“Ziara hii ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara wetu kujipatia maarifa mapya, kufungua milango ya masoko ya kimataifa, na kujifunza mbinu bora na za kisasa za uendeshaji wa biashara. Ujuzi huu utasaidia si tu kukuza biashara zao binafsi, bali pia kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema Bw. Mponzi.

 

Ameongeza kuwa, hii ni ziara ya tano tangu mwaka 2019 kufadhiliwa na Benki ya NMB kwa ajili ya wateja wake, na safari ya mwaka huu ndiyo kubwa zaidi kuwahi kufanyika, jambo linaloonesha dhamira ya benki katika kuleta matokeo chanya kwa wateja wake na taifa kwa ujumla.

Bw. Mponzi alifafanua kuwa kati ya washiriki wa mwaka huu, 12 wanatoka katika mnyororo wa thamani wa kilimo, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, huku 16 wengine wakitoka sekta mbalimbali za biashara.

Baadhi ya wafanyabiashara walioteuliwa wameeleza shukrani zao kwa NMB kwa kuwawezesha kushiriki katika programu hiyo ya kipekee.

“NMB imetufungulia milango ya ndoto zetu. Kupata nafasi kama hii ya kukutana ana kwa ana na wazalishaji wakubwa wa China ni fursa adimu,” alisema Bw. Sanjay Sumariya wa Singida Kilimo Ltd.

Naye Bi. Delfina Leon wa Barefoot International alisema kuwa anatarajia kujifunza zaidi kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa, utaratibu wa kuagiza kwa wingi, na fursa za ushirikiano wa muda mrefu na kampuni za China.

Kwa upande wake, Bw. Award Assah Mpandilah, aliyeshiriki katika ziara ya kwanza mwaka 2019, alisema:
“Nilirejea nikiwa na mtazamo mpya kabisa wa kibiashara. Kupitia ziara hiyo, niliweza kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja na wawekezaji wa China, na hadi leo tunaendeleza ushirikiano wenye mafanikio makubwa – yote haya ni matokeo ya uwekezaji wa NMB katika kuwawezesha wateja wake.”

Utaratibu huu wa NMB unaendana na ajenda ya Serikali ya kuimarisha sekta binafsi, kupanua wigo wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kimataifa, pamoja na kuvutia uwekezaji wa kigeni kupitia ushirikiano wa kimkakati.

“Kwa kutoa fursa kama hizi,” alisema Bw. David Mdeka wa Mafinga, “NMB inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuwa taasisi ya fedha na mshirika wa kweli wa maendeleo ya wateja wake na taifa kwa ujumla.”

 



No comments:

Post a Comment