Dar es Salaam. Benki ya NMB imekabidhi jezi na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi milioni 36 kwa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi), ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kukuza michezo miongoni mwa watumishi wa umma nchini.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa Shimiwi wakiongozwa na Katibu Mkuu Alex Temba na Naibu Katibu Mkuu Mariam Kihange.
Akizungumza katika tukio hilo, Meneja Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano ya Benki ya NMB na Serikali, Amanda Feruzi, alisema benki inaona michezo kama chachu ya mshikamano, afya bora, na kuongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
“NMB itaendelea kushirikiana na Shimiwi na wadau wengine kuhakikisha michezo inakuwa daraja la mshikamano na kuimarisha afya za watumishi wa umma,” alisema Feruzi.
Katika makabidhiano hayo, NMB ilikabidhi jezi, tracksuit na kombe kwa ajili ya maandalizi ya michezo inayowakutanisha Wizara na Idara za Serikali. Viongozi wa NMB walioungana na Feruzi katika tukio hilo ni Meneja NMB Kenyatta Deogratius Kawoga na Meneja Mahusiano Mwandamizi wa NMB, Josephine Kulwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shimiwi, Alex Temba, aliishukuru NMB kwa msaada huo akibainisha kuwa utasaidia kuimarisha maandalizi ya timu na kuongeza hamasa kwa washiriki wote wa michezo ya Shimiwi.
“Ushirikiano kati ya taasisi za kifedha na mashirikisho ya michezo ni kichocheo cha kukuza vipaji, mshikamano wa kijamii na kuimarisha ari ya utendaji kwa watumishi wa umma,” alisema Temba.
Michezo ya Shimiwi huandaliwa kila mwaka na hukutanisha Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwa ni jukwaa la kujenga mshikamano, afya na kuibua vipaji miongoni mwa watumishi.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment