Mwanza, Septemba 14, 2025 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa (corporates) jijini Mwanza kwa lengo la kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya, na kueleza dhamira yake ya kuanzisha dawati maalum la wataalamu wabobevu kwa ajili ya wadau wa sekta za madini, kilimo na uvuvi.
Hafla hiyo ya chakula cha jioni ilihudhuriwa na wateja wakubwa wa NBC pamoja na maofisa waandamizi wa benki hiyo, ambapo wateja walipata nafasi ya kujadili namna huduma bora na za kibunifu zinaweza kusaidia sekta zao kiuchumi.
KUZINDUA DAWATI MAALUM KWA SEKTA MUHIMU
Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NBC, Elvis Ndunguru, alisema dawati hilo litakuwa kiunganishi muhimu kati ya benki na wadau wa sekta hizo:
“Huu ni muendelezo wa matukio tuliyoanzisha ili kujadili na wateja wetu namna ya kuboresha huduma zetu kulingana na mahitaji yao. NBC tunatambua umuhimu wa kutoa huduma bora na za ubunifu kwa wateja, na dawati hili litatusaidia kuwa karibu zaidi na wadau wa sekta za madini, kilimo na uvuvi.”
Ndunguru alibainisha kuwa huduma mpya zitajumuisha mikopo, bima na elimu kuhusu uendeshaji wa kisasa wa shughuli za sekta hizo.
HUDUMA ZA KIBUNIFU KAMA NBC CONNECT
Aidha, NBC imeendelea kusogeza huduma karibu na wateja kupitia NBC Connect, jukwaa la kidigitali linalorahisisha miamala kwa taasisi na biashara kubwa, ikiwemo malipo ya ndani na ya kimataifa kwa usalama zaidi.
Bi. Nyanjige Ngambeki wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) alisema:
“NBC Connect imerahisisha sana maisha yetu, hususan katika kufanya miamala ya TISS na malipo ya nje ya nchi kwa urahisi na usalama zaidi.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Bw. Rajab Kinande, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa, aliyesisitiza kuwa huduma hiyo imeongeza ufanisi na kurahisisha shughuli za kifedha kwa taasisi nyingi.
KUELEKEA USHIRIKIANO MPANA
Kupitia mikutano kama hii, NBC inalenga:
- Kujenga mitandao ya kibiashara kati ya wateja wake
- Kutoa suluhisho za kifedha zenye ubunifu
- Kukuza ukuaji wa uchumi wa kitaifa
- Kuendeleza uwajibikaji kwa jamii kupitia elimu, afya na uhifadhi wa mazingira
Hafla hiyo pia ilihusisha maofisa wengine waandamizi wa NBC kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na makao makuu, akiwemo Msafiri Shayo, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa benki hiyo.
👉Soma zaidi kuhusu mikakati ya mabenki na maendeleo ya sekta ya kifedha kupitia Kitomari Banking & Finance Blog










No comments:
Post a Comment