DODOMA, AGOSTI 8, 2025 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imepongeza hatua ya Serikali ya kuboresha mfumo wa mauzo ya mazao ya wakulima, hususan kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambao umeziwezesha taasisi za kifedha, ikiwemo NBC, kuwafikia wakulima kwa urahisi zaidi.
Hatua hiyo imeboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kama mikopo na elimu ya fedha, na kuongeza uaminifu kati ya wakulima na taasisi za kifedha.
Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nane Nane) kitaifa jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa NBC, Bw. Raymond Urassa, alisema maboresho hayo yamerahisisha mchakato wa kuwatambua wakulima kama wateja wanaoweza kukopesheka kupitia dhamana za malipo ya mazao yao.
"Kupitia dhamana hii ya msingi, sasa tumekaribiana zaidi na wakulima," alisema Bw. Urassa.
"Kupitia akaunti ya NBC Shambani, wakulima wanaweza kupata mikopo ya nyumba bora, pembejeo na zana za kisasa za kilimo, ikiwemo matrekta, ‘power tiller’, na ‘combine harvester’. Pia wanapata mikopo ya malipo ya awali wakiwa wanasubiri malipo yao, hivyo kuepuka mikopo umiza ya mitaani. NBC tumeenda mbali zaidi kwa kuwasaidia kujenga maghala ya kuhifadhia mazao yao."
Aidha, NBC imebuni huduma za bima mahsusi kwa wakulima na wafugaji, ikiwemo bima ya afya, bima ya mifugo, na bima ya kilimo. Benki hiyo pia inashirikiana na kampuni mbalimbali ili kuwapatia wafugaji mbegu bora za mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa nyama, maziwa na mayai.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU), Bw. Karimu Chipola, alisema ushirikiano kati ya NBC na vyama vya ushirika umeleta manufaa makubwa, hasa kwa wakulima wa korosho na ufuta wa mikoa ya Mtwara na Lindi, kupitia mikopo ya zana za kilimo na elimu ya fedha.
"Sasa ni rahisi zaidi kwa vyama vya ushirika kufanikisha miamala ya wanachama kupitia akaunti zao NBC. Kupitia ushirikiano huu, tunajiandaa kujenga maghala makuu ya kuhifadhia mazao na kiwanda cha kubangua korosho," alisema Bw. Chipola.
Ushuhuda mwingine umetolewa na Bw. Maiya Saitia Maumbi, mfugaji kutoka Kilosa, Morogoro, ambaye amepokea bima ya mifugo ya NBC.
"Bima hii imetusaidia sana kukabiliana na majanga kama ukame na magonjwa ya mifugo. Sasa nafuga kwa kujiamini, nikijua nina kinga ya bima na huduma za kifedha kwa ajili ya kuboresha shughuli zangu," alisema.
Katika maonesho hayo, NBC pia ilisogeza huduma zake karibu na wananchi kupitia timu ya masoko na mawakala wake. Meneja wa NBC Tawi la Dodoma, Bi Happiness Kizigira, alisema walifanikisha ufunguzi wa akaunti nyingi kwa washiriki, huku wakipokea mwitikio mkubwa kutoka kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.










No comments:
Post a Comment