Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Monday, 28 July 2025

NMB YAMWAGA MAMILIONI KWENYE MAONYESHO YA KITAIFA YA NANE NANE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Benki ya NMB imekabidhi kiasi cha Shilingi milioni 100 kwa Wizara ya Kilimo ili kusaidia maandalizi ya Maonyesho ya Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi—maarufu kama Nane Nane—yanayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Dodoma.

Fedha hizo ni sehemu ya mchango wa zaidi ya Shilingi milioni 470 ambao NMB imekuwa ikitoa kwa maonyesho hayo kwa kipindi cha miaka saba mfululizo, ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya benki hiyo katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Bi. Janeth Shango, alisema benki hiyo itaendelea kufadhili shughuli mbalimbali za kuimarisha kilimo na ufugaji kwa lengo la kuongeza tija na kuinua uchumi wa wakulima, wafugaji na wavuvi.

“Hii siyo mara ya kwanza kushirikiana na sekta ya kilimo. Kupitia NMB Foundation, tayari tumeshawafikia zaidi ya vyama vya ushirika na AMCOS 1,500, vinavyoshughulika na mazao kama kahawa, ufuta, tumbaku na korosho,” alisema Shango.

Aliongeza kuwa fedha hizo zinakabidhiwa moja kwa moja kwa Wizara ili ziweze kuwafikia walengwa na kuboresha maisha yao kiuchumi.

“Tunaamini maendeleo ya taifa huanza na maendeleo ya wananchi wake. NMB inawawezesha wakulima kutoka kwenye kilimo cha mazoea na kuwaingiza kwenye kilimo cha kisasa chenye tija na uhakika wa soko,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Bw. Nsolo Mlozi, alisema benki hiyo huandaa kalenda ya mwaka kulingana na misimu ya kilimo, kwa lengo la kuwahudumia wakulima kwa wakati muafaka.

“Tunalenga kuwaondoa wakulima kwenye utegemezi wa mvua na kuwahamasisha kuelekea kwenye kilimo cha umwagiliaji. Pia tunawahimiza kuwa na bima za mazao na kuwaunganisha na masoko ya ndani na ya kimataifa kupitia mtandao wa NMB,” alisema Mlozi.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweri, aliishukuru NMB kwa mchango huo mkubwa na kusema utasaidia sana maandalizi ya maonyesho yatakayowakutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka sekta mbalimbali.

“Shilingi milioni 100 ni msaada mkubwa sana. Fedha hizi zitatuwezesha kuboresha miundombinu ya maonyesho pamoja na kuweka mazingira bora ya kuonesha teknolojia za kisasa za kilimo,” alisema Mweri.

Alisema NMB ni zaidi ya mfadhili, ni rafiki wa kweli wa sekta ya kilimo, na akaomba benki hiyo iendelee kushiriki pia kwenye maonyesho ya kanda katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Simiyu na Mbeya, ambako huduma za kifedha kutoka NMB zinahitajika kwa kiwango kikubwa.





No comments:

Post a Comment