Moja ya matukio makubwa nchini wakati jua linazama Jumatano wiki hii ilikuwa ni futari ya kukata na shoka iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa ajili ya watoto waishio katika mazingira magumu pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Futari ya mwaka huu iliudhuriwa pia na mawaziri, manaibu waziri, maafisa waandamizi wa serikali, viongozi wa mashirika ya umma na binafsi, makamanda wa vikosi vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, pamoja na wateja wa benki hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tabora, Bi Hawa Mwaifunga, alisema huo ni mwendekezo wa NMB kusaidia jamii na kuwa msaada huo wa kinadamu umeleta furaha, heshima, na matumaini kwa watoto hao wanaoishi kwenye mazingira magumu.
"Mchango wa Benki ya NMB kwa watoto hawa ni mkubwa na muhimu katika malezi yao. Unawsajengea utamaduni wa ukarimu na ushirikishwaji, kuhakikisha wao nao wanajihisi kuthaminiwa na kuwa sehemu ya jamii pana," alibainisha.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna, alieleza umuhimu wa Futari za NMB kwa Bunge katika kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo, wabunge, na serikali kwa ujumla.
"Kukaribishwa kwetu hapa mara kwa mara, inadhihirisha mahusiano mazuri ambayo Benki ya NMB inayo na Bunge lako Tukufu lakini zaidi na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alimwambia ngeni rasmi, Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Najma Murtaza Giga.
Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, mgeni rasmi wa hafla hiyo Bi Najma, alieleza kuwa mafanikio makubwa ya Benki ya NMB yanatokana na fadhila za ukarimu wake na baraka za ushirikiano wa kimkakati.
Alisisitiza kuwa benki hiyo si tu kwamba inajali wenye uhitaji, bali pia inadhihirisha roho ya huduma na mshikamano, ikishirikiana kwa karibu na Bunge ili kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment