Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wake, kutambuliwa huku kimataifa ni kielelezo cha wazi cha dhamira ya NMB katika kusimamia rasilimali watu kwa viwango vipya vya juu vya ajira na ustawi wa wafanyakazi wake.
Tofauti na taasisi nyingi, Benki ya NMB imeonesha kwa upekee kwamba uwekezaji madhubuti katika rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kazi ni msingi imara wa mafanikio ya kibiashara.
Kupitia programu mahiri za kuboresha afya na ustawi wa rasilimali watu, NMB si tu kwamba imeimarisha nafasi yake ya ushindani katika sekta ya huduma za kifedha, bali pia imeweka viwango vipya vya mafanikio ya muda mrefu ambavyo ni muhimu kwa taasisi yoyote yenye maono ya kimkakati.
Mapokezi hayo ya Mashujaa waliopeperusha bendera ya NMB mlimani yaliwashirikisha pia zaidi ya wafanyakazi 100 wa NMB. Benki ya NMB kila mwaka pia ina wafadhili wafanyakazi zaidi 150 kushiriki kwa hiari katika mbio za Kili Marathon ambazo ilikuimarisha ustawi wa wafanyakazi wake kimwili, kiafya, na kukuza mshikamano ndani ya taasisi.
Akiwapongeza wafanyakazi hao wanne, Bw Ngalawa alisisitiza kuwa mafanikio yao ya kupanda mlima mrefu kuliko yote barani Afrika ni ishara ya uthabiti, kujituma, na ari ya kuzishinda changamoto.
"Zoezi hili limedhihirisha kuwa NMB si tu mahali bora pa kazi, bali pia ni taasisi inayothamini na kuwekeza kikamilifu katika ustawi, maendeleo, na mafanikio ya rasilimali watu wake. Kwa kuzingatia hilo, NMB inaendelea kujenga mazingira yanayochochea ubunifu, ufanisi, na uimara wa wafanyakazi wake, hivyo kuimarisha nafasi yake kama mwajiri kinara nchini," Bw Ngalawa alibainisha.
Sifa za Utendaji Bora Ndani ya NMB
“Wafanyakazi wetu waliorejea kutoka kilele cha Mlima Kilimanjaro wametuonesha kuwa dhamira, mshikamano, na uthabiti ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo makubwa - sifa ambazo pia ndizo msingi wa utendaji bora wa benki yetu.
“Kama benki, tunaamini kuwa safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro ni kielelezo cha safari yetu ya kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na ustawi wa wafanyakazi wetu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Bw Ngalawa, Ithibati ya Mwajiri Bora Tanzania kwa Mwaka 2025 si tu ni heshima ya kusherehekewa, bali ni uthibitisho wa jitihada zao katika kuweka mifumo bora ya kazi, kushughulikia ustawi wa wafanyakazi, na kukuza utamaduni wa ushirikiano na heshima baina ya wafanyakazi wake.
Nishani hiyo, alifafanua, inaashiria kuwa Benki ya NMB imefanikiwa kuwa taasisi inayothamini rasilimali watu, kuwa na mazingira mazuri yanayohamasisha ubunifu, kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi kupitia sera bora, na kuendelea kukuza maendeleo yao kitaaluma.
“Tunapowekeza katika watu wetu, ni motisha tosha ya kufanikisha malengo yao binafsi na ya yale ya kitaasisi kwa ujumla.”
Tuzo ya Kuendelea Kupaa Juu Zaidi
Bw Ngalawa alisema katika safari ya kuwa taasisi kinara zaidi, wanawahimiza wafanyakazi kuyachukulia mafanikio haya yote kama chachu ya kuimarisha juhudi za kuboresha huduma kwa wateja na kuyafanya mazingira ya kazi kuwa mazuri zaidi.
Aidha, aliongeza kuwa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro ilibeba ujumbe wenye maana mkubwa: hakuna kizuizi kisichoweza kukabiliwa kama kuna mshikamano, nia njema na kujituma kwa dhati.
Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanadhihirisha thamani ya kufanya kazi kama timu, uvumilivu, na azma isiyotetereka katika kufanikisha malengo makubwa, ndani na nje ya mazingira ya kazi.
“Kwa pamoja, tutaendelea kupanda juu zaidi, tukiimarisha mazingira bora ya kazi, na kudumisha viwango vya juu vya ufanisi na uwajibikaji.”
Chakula cha Jioni cha Top Employers Institute Hispania
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB, Bw Emmanuel Akonaay, uthibitisho wa NMB kama Mwajiri Bora unaonesha jitihada zake za kuhakikisha ustawi wa watu wake, utamaduni shirikishi wa mahali pa kazi, na kuendelea kuboresha mbinu za usimamizi wa rasilimali watu.
Siku nne kabla ya safari ya kuelekea kilele cha Kibo, kilichopo kwenye urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari, tarehe 13 Februari, Bw Akonaay alipokea Nishani ya Mwajiri Kinara zaidi kwa niaba ya NMB katika hafla ya Top Employers Institute jijini Madrid, Hispania.
Wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Top Employers Institute, Bw David Plink, alieleza kufurahishwa kwake na mpango wa NMB wa kupeleka nishani yake hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro kama ishara ya mafanikio na ufanisi.
Bw Akonaay alimueleza kiongozi huyo kuwa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro haikuwa tu kusherehekea mafanikio ya NMB katika usimamizi wa rasilimali watu barani Afrika, bali pia juhudi za kuwahamasisha waajiri wengine kuwekeza katika ubora wa mahali pa kazi na ajira kwa ujumla.
Taasisi Inayozingatia Watu Kwanza
“Kutambulika kama Mwajiri Bora na kitendo cha kuipeleka nishani ya ithibati yake juu ya Mlima Kilimanjaro ni vielelezo tosha vya jitihada zetu za kuifanya benki yetu kuwa moja ya sehemu bora zaidi za kazi na kuendeleza vipaji duniani, na hii inadhibitisha kuwa sisi ni taasisi inayozingatia ustawi wa watu kwanza,” Bw Ngalawa alisema
Akifafanua zaidi, alieleza kuhusu programu mbalimbali zinazolenga ustawi wa wafanyakazi kwa upande wa afya ya mwili na akili, pamoja na kuwawezesha kifedha kupitia elimu ya matumizi bora ya mapato na uwekezaji wenye tija.
Alibainisha kuwa malengo haya ndiyo msingi mkuu wa kuanzishwa kwa Siku ya Ustawi wa Wafanyakazi wa NMB, ambalo jukwaa maalum linalohamasisha afya, furaha, na maendeleo ya rasilimali watu.
Uzinduzi wake ulikuwa sehemu ya kilele cha Mashindano ya Michezo ya Kikanda, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza Disemba mwaka jana, na yatakayokuwa yanafanyika kila mwaka kwa lengo la kujenga mshikamano, umoja, na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi wa NMB.
No comments:
Post a Comment