Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Thursday, 5 September 2024
NBC YASAINI MoU KUTOA HUDUMA ZENYE UPENDELEO KWA WAFUGAJI
Dar es Salaam - Septemba 5, 2024: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji na Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) yanayolenga kufungua milango na fursa kwa wafugaji na wadau walioko kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hiyo nchini ili kupata huduma za kifedha zilizo mahususi kulingana na mahitaji yao.
Hafla ya kusaini hati za makubaliano hiyo imefanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam ikihusisha viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili ambapo ilishuhudiwa Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki ya NBC, Msafiri Shayo na Katibu Mkuu wa CCWT, Mathayo Daniel wakiwasilisha taasisi zao katika kusaini makubaliano hayo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Shayo alisema hatua hiyo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kukuza na kuboresha mnyororo wa thamani wa wakulima na wafugaji nchini kupitia uwezeshaji utakaowasaidia wadau hao kuendesha shughuli zao kisasa zaidi sambamba na kuongeza vipato na ajira, lengo likiwa ni kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Zaidi tunalenga kuongeza upatikanaji wa chakula na lishe itokanayo na sekta hii muhimu ambapo kupitia huduma zetu mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo tunalenga kuwawezesha wadau wa sekta hii ili waweze kutimiza wajibu wao kikamilifu kwa kuboresha ufanisi wao katika shughuli zao ikiwemo biashara,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Shayo kupitia makubaliano hayo, wafugaji watakaojiunga na huduma ya Mfugaji Akaunti inayotolewa na benki hiyo mahususi kwa ajili yao wataweza kunufaika na faida mbalimbali ikiwemo mikopo kwa ajili ya uendelazaji shughuli zao ikiwemo biashara, huku pia wakinufaika na riba ya faida kwa salio la akiba linalozidi kiasi cha Sh 100,000 kila mwezi, kufungua akaunti bure ambayo haina makato ya uendeshaji kila mwezi.
“Zaidi wafugaji watapata bima mbali mbali ikiwemo bima ya ufugaji na bima ya afya, watapatiwa taarifa za akaunti bila makato, gharama nafuu za utoaji wa fedha kiasi chochote wakati wowote, huduma za kibenki kwa njia ya simu (NBC Kiganjani) pamoja na kupatiwa kadi ya NBC Visa itakayowawezesha kutoa pesa kwenye ATM yoyote duniani yenye kukubali kadi ya Visa au kulipia huduma za mtandaoni na mashine za malipo madukani,’’ alitaja.
Akifafanua zaidi kuhusu hatua hiyo, Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa alisema itachochea ukuaji wa sekta ya mifugo nchini kwa kuwa kupitia mpango huo, pamoja na faida nyingine nyingi benki hiyo inalenga kuwawezesha wafugaji kwa kuwapatia mikopo itakayowasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji na ubora wa bidhaa zao.
“Kupitia mikopo watakayopata wadau hawa wa sekta hii ya ufugaji, wataweza kunenepesha zaidi mifugo yao, wataongeza uzalishaji wa maziwa, watazalisha mbegu bora, wataweza kumudu gharama za malisho bora kwa mifugo yao, wataweza kumudu gharama za matibabu kwa mifugo yao na wao binafsi pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali inayohusiana na uwekezaji wao ikiwemo mabwawa ya kuogeshea mifugo (majosho),’’ alisema.
Kwa upande wake Bw. Mathayo pamoja na kuipongeza na kuishukuru benki hiyo kwa kulikumbuka kundi hilo muhimu alisema ujio wa huduma hizo mahususi kwa ajili yao, utawasaidia kwa kiasi kikubwa wadau mbalimbali wa sekta ya ufugaji nchini kuongeza ufanisi na ubora wa shughuli zao hatua ambayo itachochea kwa kiasi kikubwa uzalishaji na ukuaji wa uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.
“Kupitia upendeleo huu tutakaopata kupitia benki ya NBC ikiwemo huduma za mikopo, elimu ya fedha na huduma nyingine ikiwemo bima za afya tunatarajia kwamba kasi ya uzalishaji wetu itaongezeka huku pia tukiwa na uhakika wa kuzalisha bidhaa zilizo bora zaidi kwa faida ya wateja wetu na jamii kwa ujumla…tunawashukuru sana NBC ni wakati wetu sasa kuchangamkia fursa hii,’’ alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment