BURUNDI, DRC ZAFURAHIA CRDB BANK MARATHON KUVUKA MIPAKA, SHILINGI BILIONI 2 KUKUSANYWA
Dar es Salaam, Tanzania - 9 Julai 2024: Nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha CRDB Bank Marathon katika nchi zao. Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Leontine Nzeyimana, na Mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchini, Patrice Tshekoya wakisisitiza umuhimu wa mbio hizo katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi hizo.
“Benki ya CRDB imeonyesha ni kwa namna gani si tu ipo kibiashara bali pia inajali jamii. Tunawashukuru kwa moyo wenu huu wa kujitoa. Kwa miaka zaidi ya 10 ambayo Benki hii imekuwa nchini Burundi imekuwa na mchango mkubwa katika kuchcochea maendeleo. Burundi na Tanzania ni ndugu, na Benki ya CRDB nchini Burundi ipo nyumbani, hivyo hata marathon hii pia imefika nyumbani,” amesema Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Leontine Nzeyimana.
Akizungumza kwaniaba ya Serikali ya Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, ameipongeza Benki ya CRDB kwa uamuzi wa kufanya CRDB Bank Marathon katika nchi tatu, akisema jitihada hizo zinaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Group, Abdulmajid Nsekela, alisema kuwa upanuzi wa CRDB Bank Marathon katika nchi za DRC na Burundi unakwenda sambamba na malengo ya benki ya kujitanua kikanda na kuchochea maendeleo barani Afrika. Nsekela alisema Benki ya CRDB imejipanga kikamilifu kusaidia kuweka mazingira wezeshi na kuwawezesha wananchi katika nchi inapotoa huduma kunufaika na fursa malengo ya Afrika Tuitakayo “The Africa We Want” 2063.
"Benki ya CRDB imefanikiwa kufikia mafanikio makubwa katika nchi za DRC na Burundi kutokana na mahusiano mazuri baina ya Tanzania na nchi hizo, yakichagizwa na uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimiye, na Rais wa DRC Congo, Mhe. FĂ©lix Tshisekedi," alisema Nsekela.
Malengo ya msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon ni kusajili wanajeshi wa kusambaza tabasamu (washiriki) zaidi ya 8,000 na kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 2. Katika msimu huu, CRDB Bank Marathon inatarajia kuanza jijini Lubumbashi nchini DRC Agosti 4, kisha kuelekea jijini Bunjumbura nchini Burundi Agosti 11 kabla ya kurudi Dar es Salaam Agosti 18.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa ambaye ndiye Kamanda wa Jeshi la Kusambaza Tabasamu (JLKT) la CRDB Bank Marathon, alisema mbali na makundi ambayo yamekuwa yakinufaika na mbio hizo ikiwamo watoto wenye maradhi ya moyo na wakinamama wenye ujauzito hatarishi na fistula, mwaka huu sehemu ya fedha zitakazokusanywa zitakwenda kusaidia jitihada za kuwajengea uwezo vijana nchini.
"Takwimu za Sensa ya Mwaka 2022 zinaonyesha vijana ni asilimia 75 ya Idadi ya Watanzania wote. Inakadiriwa kuwa takriban vijana milioni 1 wanaingia katika soko la ajira la Tanzania kila mwaka. Vijana wanapowezeshwa, wanaweza kuwa nguvu ya kubadilisha jamii kwa njia chanya, kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa kiuchumi, kukuza uvumbuzi, na kujenga mazingira endelevu kwa ajili ya siku zijazo," alisema Tully.
Katika utekelezaji wa mpango huo wa uwezeshaji wa vijana kupitia CRDB Bank Marathon, Benki ya CRDB pia imekabidhi msaada wa fedha kwa timu ya Taifa ya Olympic kushiriki katika Mashindano ya Olympic yatakayofanyika Paris, Ufaransa kuanzia tarehe 26 Julai hadi 11 Agosti 2024. Akikabidhi hundi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Group, Abdulmajid Nsekela alisema, "Uwezeshaji wa timu hiyo ya Taifa ya Olympic ni hatua muhimu ya kuwaweka vijana katika ramani ya kimataifa, ikitoa njia ya mafanikio kwao binafsi, familia zao, na jamii kwa ujumla."
Katika ripoti iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, imeelezwa kuwa katika misimu minne iliyopita, CRDB Bank Marathon imekusanya shilingi bilioni 2.7 ambazo zilielekezwa katika kusaidia upasuaji kwa watoto zaidi ya 300 wenye maradhi ya moyo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wakinamama wenye ujauzito hatarishi zaidi 150 Hospitali ya CCBRT, ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI), ujenzi wa Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto Zanzibar, na kampeni ya utunzaji mazingira ya ‘Pendezesha Tanzania’. Zaidi ya wakimbiaji 12,000 wameweza kushiriki wakiwa sehemu ya Jeshi la Kusambaza Tabasamu (JLKT).
No comments:
Post a Comment