Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday, 18 October 2023

NIC INSURANCE YAADHIMISHA MIAKA 60, HUDUMA ZA BIMA


Dar es Salaam - Oktoba 17, 2023: Katika kusherehekea kuwahudumia wateja na huduma bora za viwango vya hali ya juu, shirika kongwe la huduma za bima Tanzania, limeadhimisha miaka 60 tangu kuanza shughuli zake nchini.


Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu yake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Insurance, Dkt. Elirehema Doriye amepongeza wafanyakazi na wateja kwa kutambua mchango wao katika kulifanya shirika kuendelea kutoa huduma bunifu na za viwango vya juu kwenye sekta ya bima.


“Wateja ndio sababu kubwa kwa taasisi yoyote duniani iwe binafsi au ya umma kwasababu wao ndio sababu ya pekee kuwepo kwetu tukijituma kwa bidii ili kuwatimizia mahitaji yao. Ninajisikia fahari kubwa kuongoza kampuni ambayo ina wateja waaminifu wanaotumia huduma zetu za bima kwa miaka mingi katika shughuli zao za kila siku nchini Tanzania. Mafanikio tuliyonayo sasa yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kutoa huduma za bima zenye ushindani mkubwa kwa kuzingatia mabadiliko katika sekta yanayoendeshwa na maendeleo ya kidigitali,” alisema Dkt. Doriye.

NIC Insurance ilianzishwa Oktoba 16, 1963 ambapo serikali ilikuwa inamilika hisa kwa asilimia 51 na zilizobakia za asilimia 49 zikimilikiwa na makampuni ya Munich-Re, Swiss-Re na Colin Hood Insurance Brokers Limited.

Baada ya Azimio la Arusha mnamo Februari 1967, shirika hili lilitaifishwa na kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na ilikuwa ni kampuni pekee ya bima kwa muda wa miaka 30. Lakini mwaka 1996, sekta ya huduma za bima ikafanywa kuwa huria na kuruhusu wadau wengine kuanza kutoa huduma hivyo kupelekea ushindani tulionao sasa tukishuhudia ubunifu wa aina tofauti ili kukidhi mahitaji ya Watanzania nchini kote.

“Kutimiza miaka 60 ina maana kubwa kwa shirika letu ambalo ni kongwe au naweza kusema waanzilishi wa utoaji wa huduma za bima nchini Tanzania. Uwepo wetu kwa miaka yote hii ni dhahiri kuwa tumeshuhudia sekta hii ikianza, mabadiliko yake na mpaka sasa ambapo ushindani umekuwa mkubwa. Hivi ninavyozungumza, tumekwishatoa huduma za bima zaidi ya 3,500, tukifanya kazi na makampuni zaidi ya 200, huku madai ya wateja zaidi ya 5,000 yakitimizwa. Tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini, katika shamrashamra hizi tutakuwa na shughuli tofauti zitakazoambatana na zawadi kemkem,” alimalizia Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Insurance.

Miaka 60 ya NIC Insurance katika sekta ya bima nchini imeaambatana na mafanikio mbalimbali ikiwemo kutambuliwa kwa Utendaji Bora Katika Sekta za Fedha, Cheti cha Utambulisho cha Ubora wa Kimataifa (ISO), pamoja na kutambuliwa na Superbrands kama kampuni bora ya huduma za bima katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Pia kumelifanya shirika kuendelea kuaminika zaidi miongoni mwa wateja na washirika wake na kuwavutia wadau wengine kutaka kufanya kazi pamoja. Hivi karibuni ilizindua ushirikiano na Klabu ya Yangu, kwa kudhamini kipengele cha tunzo ya mchezaji bora wa mwezi kwa misimu mitatu mpaka 2026.

No comments:

Post a Comment