Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday, 16 October 2023

MSAFARA WA TWENDE BUTIAMA WAKAMILIKA KWA MAFANIKO


Butiama - Oktoba 14, 2023: Baada ya safari ya siku 14, zaidi ya kilometa 1,500 kupita wilaya 20 za mikoa 10 tofauti nchini, hatimaye msafara wa waendesha baiskeli wa Twende Butiama umetamatisha ziara yake iliyoanza Oktoba mosi jijini Dar es Salaam na kuwasili Mwitongo, Butiama Oktoba 14, ikiwa ni jitihada za kuenzi maisha na urithi aliotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.


Akizungumza wakati wa kuupokea msafara huo nyumbani alikozaliwa Mwalimu Nyerere wilayani Butiama, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Gerson Msigwa amepongeza juhudi za waendesha baiskeli wa msafara wa Twende Butiama kwa kutimiza adhma yao waliyojiwekea wakati wanaanza safari yao Dar es Salaam kwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo kupitia utekelezaji wa shughuli za kielimu, afya, na mazingira.


“Nichukue fursa hii kuwapongeza waendesha baiskeli wa msafara wa Twende Butiama na uongozi mzima kwa ushujaa wa kipekee kuweza kufanikisha ziara hii. Waendesha baiskeli 75, wakiwemo wazee na watoto wameendesha Siku 14, kilomita zaidi ya 1,500 kukatisha mikoa 10 na wilaya 20 ni jambo la kujivunia na mnastahili pongezi za dhati na mfano wa kuigwa na jamii nzima. Lakini, cha kujivunia zaidi ni kwamba mliamua kutumia msafara huu wa baiskeli kumuenzi baba wa taifa.

 
 
Kuhusu umuhimu wa kuhamasisha shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia michezo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo aliongezea zaidi kuwa kuendesha baiskeli sio tu kama chombo cha usafiri pekee bali pia ni mazoezi tosha kiafya kwa sababu viungo vya mwili mzima vinakuwa vinahusika ili kukutoa sehemu kwenda nyingine.


“Kwa wasiofahamu, Baba wa Taifa alikuwa mpenzi wa kuendesha baiskeli katika muda wake ambao hakuwa anafanya majukumu ya kitaifa. Hivyo, nimefurahishwa na namna mlivyochagua jambo hili kama kumuenzi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa shughuli ambazo alikuwa anazithamini na kuzipambania ikiwemo elimu, kupambana na maradhi, pamoja na utunzaji wa mazingira. Kupitia madawati mliyochangia watoto wetu wataweza kusoma vizuri, miti mliyoipanda itasaidia kuokoa mazingira yetu, kutoa kivuli na matunda, lakini pia msaada wa vifaatiba na kambi za matibabu ya bure mlizoziendesha zitawanufaisha wakazi wa maeneo husika kwa siku nyingi zijazo. Niwapongeze tena, na kuwatia moyo kuwa juhudi hizi ziweze kuendelea kufanyika kila mwaka, niwashauri watanzania wenzangu kuwaunga mkono. Sisi kama serikali tunatambua mchango wenu, na tunawaomba wadau kama Vodacom Tanzania Foundation kuendelea kujitokeza zaidi katika kuwadhamini ili mzidi kupanua wigo wa shughuli zenu nchini kote,” alihitimisha Mh. Msigwa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC. Bw. Athumani Mlinga aliwapongeza waandaji na washiriki wote wa msafara wa Twende Butiama kwa kuweza kutimiza malengo waliyojiwekea tangu kuanza kwa safari yao jijini Dar es Salaam pamoja na kuendeleza shughuli hii kwa mwaka wa tano bila kuchoka.


“Msafara wa Twende Butiama ni mfano wa kuigwa kwa ubunifu wao kwa kutumia zoezi la kuendesha baiskeli kutekeleza shughuli muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Kama Vodacom Tanzania Foundation, tumekuwa tukishiriki katika miradi mbalimbali ya kijamii tukiunga mkono serikali katika kuwanufaisha Watanzania wote. Tuliona dhamira ya dhati kupitia tukio hili ambalo lengo lake kuu ni kumuenzia Mwalimu Nyerere kwa vitendo, na huo ndio utofauti tuliouona,” aliongezea Bw. Mlinga.

Kwa kumalizia Mkurugenzi huyo wa TEHAMA alisema, “kwa kweli tunawashukuru sana waendesha baiskeli wa Twende Butima kwa kutuonyesha njia sahihi ya kumuenzi baba wa taifa na kutunza uridhi wake. Kupitia ubia huu tumeweza kuwagusa watanzania wenzetu kwa kukabidhi takriban madawati 610 kwa shule 13 na kufanikisha kuchangisha fedha zitakachotumika kununua madawati na kunufaisha wanafunzi wetu ili waweze kujisomea bila ya changamoto. Pia, tumeweza kupanda miti 6,000 na kuchangia ikiwa tumefikia na kuvuka lengo tulilojiwekea kwa mwaka huu. Kwa upande wa afya, tumeendesha kambi ya matibabu ya bure kwa kushirikiana na madaktari wa Afya Check ambapo zaidi ya wakazi zaidi ya 3000 wa maeneo ya Mwanza, Bunda na Butiama wamenufaika. Na kwa kuhitimisha ziara yetu, tumekabidhi msaada wa vifaa tiba kwa hospitali ya Wilaya ya Butiama ili kusaidia uboreshaji wa huduma za kiafya kwa kweli tumefurahi - Nyerere Day ya mwaka huu imekuwa ya furaha sana kwetu Vodacom.”

Kwa kumalizia, Mwenyekiti wa Twende Butiama, Bw. Gabriel Landa alishukuru ushirikiano walioupata kutoka kwa wadau mbalimbali katika msafara huu wa mwaka 2023 ikiwemo serikali na taasisi zake, watanzania waliotoa michango yao, wabia wa msafara wa Twende Butima pamoja na walimu, wazazi, na wanafunzi.

“Shughuli ya mwaka huu imekuwa ni yenye mafanikio makubwa kutokana na mwitikio mkubwa kutoka kwa washiriki takribani 200, kuungwa mkono zaidi na serikali, lakini pia udhamini mkubwa wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation. Hivyo, tumeweza kutekeleza kwa kiasi kikubwa zoezi la kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa utekelezaji mkubwa wa shughuli ambazo alikuwa anazithamini kwa dhati. Tunaamini kuwa Watanzania wengi zaidi katika maeneo ambayo tumepita watanufaika na shughuli tulizozifanya kwa miaka mingi ijayo. Niishukuru serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa, na Michezo kwa kuwa nasi tangu uzinduzi wa msafara huu, washiriki wote ambao tumemaliza safari kama tulivyodhamiria, bila shaka mwakani tutatekeleza zaidi ya malengo ya mwaka huu,” alimalizia Bw. Landa.

No comments:

Post a Comment