Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo cha uratibu wa rufaa na usafiri wa dharura (dispatch center) cha m-mama kilichopo katika hospitali ya rufaa ya Mount Meru, Afisa Elimu wa Mkoa Abel Tupwa aliyemuwakilisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. John Mongella amepongeza mafanikio yanayoonekana kutokana na mpango huo kwenye kila mkoa ambao umetambulishwa kwa kusaidia kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga.
“m-mama ni matokeo chanya ya ushirikiano wa serikali na sekta binafsi kwa kutoa suluhisho za kibunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Mfumo huu unatumia teknolojia rahisi na ya kisasa kabisa kuratibu rufaa na kuwarahisishia akina mama wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga kupata huduma ya usafiri wa dharura ili kuwahishwa kwenye kituo kinachoweza kutoa huduma stahiki. Mfumo wa m-mama unawezeshwa na mtandao mpana wa hospitali za serikali, ambulansi za serikali na wamiliki wa magari binafsi almaarufu madereva jamii na teknolojia iliyobuniwa na kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kutatua changamoto ya usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga kupitia mfumo huu unaowaunganisha watoa huduma za afya kwa pamoja” alisema Bw Tupwa.
Afisa Elimu wa Mkoa aliongezea kuwa, “Takwimu za wizara ya Afya zinaonesha tunapoteza akinamama 250 katika kila vizazi hai 100,000, na watoto wachanga 25 katika kila vizazi hai 1,000. Tukiiutekeleza vizuri mfumo wa m-mama tutapunguza vifo vya akinamama wajawazito na waliojifungua kwa asilimia 38% na watoto wachanga kwa asilimia 47. Naomba nitoe wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuutumia mfumo huu ipasavyo kwani kuna uwezekano mkubwa kila mmiliki wa gari unayemuona mtaani kwako akawa msaada wa kutoa usafiri wa dharura pindi unapopata dharura ya mjamzito, aliyejifungua na mtoto mchanga. Lakini pia nawasihi madereva magari binafsi muunge jitihada hizi za serikali na Vodacom katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi mkoani kwetu.”
Akifafanua ubunifu nyuma ya mfumo wa m-mama na jinsi unavyofanya kazi, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Vodacom Tanzania Plc, George Venanty alisema kuwa, “Vodacom kwa kushirikiana na serikali, tumetumia ujuzi wetu katika maswala ya teknolojia kuja na mfumo unaoiwezesha serikali kushughulikia dharura na rufaa kwa upesi kwani unawapa uwezo wa kuwaunganisha kina mama wenye dharura au vichanga vyao na ambulensi za serikali au madereva jamii kupitia kituo cha uratibu wa rufaa na usafiri wa dharura (dispatch center) zinazoendesha na serikali kama hii tuliyoiona hapa leo na hivyo kumuwezesha mama au mtoto kufikishwa katika kituo cha afya husika kwa wakati na hivyo kuokoa maisha yao. Haya yote yanawezeshwa na mtandao wetu mawasiliano ulioenea nchi nzima alisema Venanty.
Utafiti wa majaribio ya mfumo wa m-mama ulianza kufanyika katika mikoa ua Mwanza na Shinyanga mnamo mwaka 2013 hadi 2021 ukilenga kutatua tatizo la akina mama wajawazito kutokuwa na usafiri na kuchelewa kujifungua. Huduma hii ilichangia kupunguza vifo vitokanavyo na kuchelewa kupata huduma kwa sababu ya ukosefu wa usafiri wa dharura kwa asilimia 38 na kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 47 ndani ya kipindi hicho mkoani Shinyanga.
Kupitia mfumo wa m-mama zaidi ya akinamama na watoto wachanga 18,600 wamesafikirishwa (wanawake 15,559 na Watoto wachanga 3,131) hii ikiwa ni Tanzania bara na Zanzibar. Kwa kuzingatia ushirikiano endelevu baina ya serikali na Vodacom Tanzania Plc, gharama zote za uendeshaji na usafirishaji zinasimamiwa kikamilifu ndani ya bajeti za serikali.
Mpaka sasa mfumo wa m-mama unafanya kazi kwa ukamilifu kwenye mikoa 8 kwa Tanzania Bara na na mikoa yote mitano ya Tanzania Zanzibar. Mfumo huu utatekelezwa nchi nzima ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment