Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Friday 21 October 2022

14 NOVEMBA 2022 NI UZINDUZI WA SERA YA UBIA YA NHC


Dodoma, 20 Oktoba 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI- NOVEMBA 14 NI UZINDUZI WA SERA YA UBIA YA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
  1. Ndugu zangu Waandishi wa Habari, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana nanyi siku hii ya leo tukiwa na afya njema. Ndugu zangu Waandishi wa Habari tumewaita hapa leo kwa ajili ya kuwaeleza matayarisho tuliyokwishafanya ya uzinduzi wa sera ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa.
  2. Kama mnakumbuka, Oktoba 21 tuliwaeleza kuwa Shirika la Nyumba la Taifa linaenda kuzindua sera yake ya ubia. Hata hivyo, baada ya kuanza kuutangazia umma juu ya jambo hilo jema, kumekuwa na muitikio mkubwa wa makampuni binafsi ya ndani na nje ya nchi wa kushiriki uzinduzi huo. Aidha, yameletwa maombi mengi ya Diaspora na wawekezaji wa Kimataifa kutaka kuhudhuria uzinduzi huo nchini Tanzania. 
  3. Ndugu Wanahabari, ni kutokana na maombi hayo, Shirika limeamua sasa kusogeza mbele tarehe ya uzinduzi huo ili kuruhusu idadi hiyo kubwa ya wanaotaka kuwekeza katika sekta ya nyumba nchini waweze kushiriki. Hivyo, napenda kuwafahamisheni kwamba Shirika la Nyumba la Taifa litazindua Sera yake ya ubia tarehe 14 Novemba, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Uzinduzi wa sera hii iliyoboreshwa una maslahi mapana kwa Shirika, wawekezaji na Taifa kwa ujumla na unalenga kuwapatia fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini. 
  4. Kauli mbiu ya uzinduzi wa sera hii ni “Tunajenga Taifa letu kwa Ubia na Sekta Binafsi”. Kauli mbiu hii inahimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza maeneo yaliyopo katikati ya miji ambayo yana thamani kubwa kuliko majengo majengo yaliyopo sasa, ili kukuza mapato ya Shirika.
  5. Ndugu Wanahabari, uzinduzi wa Sera ya Ubia unaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kwa hakika tunaunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta maendeleo ili iwekeze mitaji yao kujenga uchumi wa Taifa letu. 
  6. Ndugu Wanahabari, sera ya ubia ambayo tunawaalika Wawekezaji kushiriki ilianzishwa na Shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika. Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 na yamezingatia kuvutia uwekezaji kwa kuwa yana maslahi kwa Shirika na mwekezaji. Tangu kuanza kwa utaratibu huu, jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya TZS Bilioni 300. Katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika na miradi 30 yenye thamani ya TZS Bilioni 60 inaendelea kukamilishwa. 
  7. Miradi hii imechangia upatikanaji wa ajira, kuboresha mandhari ya miji yetu, kuongeza mapato ya Shirika, kuongeza wigo wa kodi za serikali, kuongeza maeneo kwa ajili ya biashara na makazi na kuipanga miji yetu
  8. Katika uzinduzi huu mkubwa tunakusudia kuwa na washiriki takribani 1,000 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi; vyama na bodi za kitaaluma pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao wamealikwa. Aidha, mabalozi wa nchi zenye wawekezaji wakubwa wamealikwa na wawakilishi wa Kamati za Bunge zinazogusa shughuli za Shirika wamealikwa.
  9. Ndugu zangu Wanahabari, niwashukuru sana kwa ushirikiano wenu mnaotupatia mara kwa mara. Niwakaribishe muendelee kutuunga mkono na sisi tutakuwa pamoja nanyi kila inapohitajika ili muweze kufahamu kinachofanywa na Shirika lenu la Nyumba la Taifa. Kwa mawasiliano zaidi juu ya kushiriki kwenye uzinduzi huo tafadhali piga simu nambari +255 767 566 299 au +255 658 662 800 au tutumie ujumbe kupitia baruapepe nhcjv@nhc.co.tz
IMETOLEWA NA:
MUUNGANO SAGUYA,                                                      
MENEJA HABARI NA UHUSIANO,
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA.

No comments:

Post a Comment