Baadhi ya wafanyabiashara wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizotolewa katika hafla ya ufunguzi wa NMB Business Club iliyofanyika Katika ukumbi wa Sea View Beach Resort iliyopo Mkoani Lindi. |
Kwa mara ya kwanza wakulima, wavuvi na wafugaji nchini wataweza kupata mikopo kutoka Benki ya NMB kwa riba nafuu kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao, baada ya taasisi hiyo kupunguza riba hadi asilimia tisa.
Hatua ya benki hiyo kupunguza riba ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyotoa mwaka huu kwa taasisi za kifedha kupunguza riba hadi kufikia namba moja (Single Digit).
Kaimu Afisa Mkuu wa Udhibiti na Utekelezaji wa Benki ya NMB, Ndg. Oscar Nyirenda alisema kuwa NMB imepunguza riba ya mikopo kwa sekta mama za kilimo, uvuvi na ufugaji hadi kufikia asilimia tisa mwaka 2022.
Alisema kuanzia Julai, 2021 hadi Juni 2022 jumla ya mikopo 37,500 yenye thamani ya Sh bilioni 752.7 imetolewa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za biashara.
Aliongezea kuwa kushuka kwa riba kumesababisha idadi ya wafanyabiashara wanaokopa katika benki hiyo kuongezeka kulinganisha na miaka ya nyuma kabla ya NMB kupunguza kwa kiwango hicho cha riba ya mikopo yake.
Meneja wa NMB Kanda ya kusini, Janeth Shango alisema benki hiyo iko tayari kuwahudumia wafanyabiashara katika mitaji na elimu ili huduma zao ziwe na ufanisi na faida kwao pia.
Mwenyekiti wa klabu ya wafanyabiashara ya benki hiyo Mkoa wa Mtwara, Hamisi Bandari alisema kuwa changamoto walizonazo ni pamoja na kutokuwa na elimu ya masuala ya kodi, utunzaji na usimamizi wa fedha na hofu ya kutafuta mitaji.
Lakini pia, aliwataka wafanyabaishara wa Mtwara kujipanga kuchangamkia fursa za kibiashara zinazofunguka hususani za visiwa vya Comoro na wenye mitaji midogo kufika Benki ya NMB kuomba mikopo.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Lindi, Hamis Livembe aliiomba serikali pamoja na taasisi za kifedha kuwatengenezea mazingira mazuri ya kifedha ili waweze kushiriki katika miradi mikubwa iliyopo mkoani humo mfano mradi mkubwa wa gesi LNG ambao unaashiria mabadiliko makubwa ya kimaendeleao mkoani Lindi.
No comments:
Post a Comment