Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, akizungumza kabla ya kufungwa kwa kongamano la wiki ya ununuzi wa umma, iliyohusisha wadau wa ununuzi wa umma na Ugavi nchini, jijini Arusha. |
Na. Saidina Msangi, WFM, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, amewataka wataalam wa ununuzi na ugavi pamoja na wadau wote wanaohusika kwenye michakato ya ununuzi kuzingatia misingi ya uadilifu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Maagizo hayo aliyatoa Meya wa jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iranghe, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Bw. John Mongela, wakati wa kufunga Kongamano la Wiki ya ununuzi wa umma lililowakutanisha wadau wa ununuzi takribani 1,000 wakiwemo maafisa ugavi, wazabuni, wajumbe wa bodi na maafisa masuuli kutoka Wizara, taasisi, Halmashauri na sekta binafsi.
Alisema kuwa sheria nzuri pamoja na mifumo mizuri ya Tehama, haitakuwa na maana kama wanaohusika kwenye michakato ya ununuzi hawatazingatia miiko ya taaluma zao, uadilifu na uzalendo.
"Hatutarajii kuwepo na mtaalamu yeyote atakayeenda kinyume na matarajio na maono ya Serikali katika dhana ya kukuza uchumi wa viwanda. Yeyote atakayepata nafasi yoyote ya kiutendaji, anapaswa kufanya maamuzi yatakayoisaidia Serikali hii kufikia matarajio hayo na sio kuwa kikwazo’’alisema Mhe. Iranghe.
Alisisitiza kuwa kwa yeyote atakayefanya hila au ujanja unaoweza kukwamisha juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa nchi na kutoa huduma bora kwa wananchi, asifumbiwe macho wala kuhurumiwa kwa namna yoyote ile ili kuleta nidhamu ya kazi na kuongeza tija na uwajibikaji.
Aidha, ametoa rai kwa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), kusimamia vizuri ukidhi wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ili sekta hiyo iondokane na dhana ya kuwa kichaka cha wezi wa fedha za walipa kodi.
Amesema PPRA iendelee kufanya kaguzi na kuhakikisha wale wote wanaokiuka maadili na miiko ya taaluma zao ni vema wakafikishwa katika Bodi zao za taaluma kama vile PSPTB, ERB, CRB na nyinginezo ili washughulikiwe kwa mujibu wa misingi ya taaluma zao.
Aidha alisisitiza waandaaji wa kongamano hilo kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Kasimu Majaliwa, wakati akifunguaKongamano hilo.
‘’Nyie ndio wasimamizi wakubwa wa sekta hii ya Ununuzi wa Umma hapa nchini. Serikali na Watanzania wanawategemea sana katika kuhakikisha kuwa fedha za walipakodi zinazoelekezwa katika ununuzi wa bidhaa, huduma na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika ipasavyo na kama ilivyopangwa’’, alisema Dkt. Mongela.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Ununuzi wa Umma Dkt. Irene Isaka, alisema kuwa kongamano hilo limetoa fursa kwa Wadau wa Ununuzi wa Umma na Ugavi kupata elimu, kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu utekelezaji wa shughuli za ununuzi.
"Tunaamini washiriki wamefaidika sana na mijadala iliyotokana na mada 15 ambazo ziliwasilishwa na watoa mada mahiri. Ni matarajio ya waandaaji wa Kongamano hili washiriki wote watakuwa mabalozi wazuri wa mawazo chanya waliyoyapata kwa wakati wote wa kongamano hili’’ alisema Dk. Isaka.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na Hatua iliyofikiwa katika Utekelezaji wa Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (TANePS), mafanikio na changamoto, matumizi ya mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao, uzoefu kutoka taasisi nunuzi, matumizi ya mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa fedha za Uviko – 19.
No comments:
Post a Comment