Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati), akifuatilia kwa umakini Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili kuhusu bajeti ya Jumuiya hiyo pamoja na kujaza nafasi za ajira katika Jumyuiya hiyo, Jijini Arusha. |
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, (kushoto), akifuatilia kwa umakini Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili kuhusu bajeti ya Jumuiya hiyo pamoja na kujaza nafasi za ajira katika Jumyuiya hiyo, Jijini Arusha. |
Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limetoa mapendekezo ya bajeti ya jumla ya dola za Marekani milioni 91.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 37.5 zinatarajiwa kutolewa na wadau wa maendeleo.
Mapendekezo hayo yametolewa kwenye Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha.
Akizungumza kuhusu Mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa Bajeti inayopendekezwa imezingatia kubana matumizi na kuelekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Mapendekezo ya Bajeti ya Jumuiya hiyo inayoundwa na nchi sita wanachama, ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ni sawa na Bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2021/2022 na yamebaki hivyo kutokana na changamoto inayopitiwa na Nchi Wanachama katika kukabiliana na madhara ya UVIKO-19.
Baraza hilo limependekeza kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 54.1 kitumike kwa ajili ya mihimili ya Sekretarieti ikiwemo Mahakama ya Afrika Mashariki, Bunge la Afrika Mashariki na Taasisi zake ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASTECO) na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).
Taasisi nyingine ni Tume ya Kiswahili (EAKC), Tume ya Utafiti wa Afya (EAHRC) na Mamlaka ya Ushindani ya Jumuiya hiyo (EACA); dola za Marekani 644,219 ni kwa ajili ya Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA) na dola za Marekani 465,500 zitaelekezwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO).
Aidha, Baraza hilo Maalum la Mawaziri limependekeza Bajeti ya mwaka 2022/2023 igharamie utekelezaji wa miradi ndani ya Jumuiya, ikiwemo, awamu ya pili ya Ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), Matengenezo ya Meli ya Utafiti katika Ziwa Victoria ijulikanayo kama RV Jumuiya, Ujenzi wa Awamu ya Pili ya Makao Makuu ya Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na Kuwezesha zoezi la uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya.
Aidha, Mkutano huo Maalum wa 47 wa Baraza Maalum la Mawaziri wa EAC umepitia na kujadili taarifa ya Kamati ya Fedha na Utawala na Taarifa ya matokeo ya zoezi la usaili wa watumishi wapya wanaotarajiwa kuajiriwa katika Jumuiya hiyo.
Mkutano huo Maalum ulitanguliwa na mikutano ya awali ambayo ni; Mkutano Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 4 Aprili 2022 na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 5 Aprili 2022.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambaye ameambatana na; Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa.
No comments:
Post a Comment