Makamu Mwenyekiti wa Umoja Switch, Godfrey Ndalahwa. |
Taasisi za kifedha zinazotumia mfumo mmoja wa malipo wa Umoja Switch zimejipanga kuboresha mfumo huo kwa kutumia teknolojia za kisasa zaidi ili kuweza kuleta tija kwa wateja wao.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa wadau wa Umoja Switch, Makamu Mwenyekiti wa Umoja Switch, Godfrey Ndalahwa alisema taasisi ya Umoja iliyoanza miaka 15 iliyopita inashirikia benki wanachama 20 na awali ikijulikana zaidi kuendesha mfumo wa Umoja Switch maalumu kwa matumizi ya kadi za ATM.
Bwana Ndalahwa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kuona ni kwa namna gani wanaweza kuboresha mfumo huo na kuangalia suala la kupunguza gharama za huduma ndani ya mfumo ili kuwafanya wateja waone faida ya kutumia mfumo huo.
“Licha ya kuwa mfumo uliozoeleka ni wa ATM za Umoja, bado kuna mifumo ya wakala, simu za mkononi na mingineyo ambayo yote inatumia teknolojia, mazungumzo ya leo yanalenga zaidi ni namna gani tunaweza kutumia teknlojia katika kuboresha mifumo yetu kwa faida ya wateja wetu”, alisema Bwana Ndalahwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch, Miriam Malima alisema mkakati wao katika mwaka huu ni kuzifikia benki zote ndogo na kubwa kama sehemu ya azma ya Umoja Switch kufikisha huhuma za kibenki kwa mtanzania aliyeko kijijini kwa gharama nafuu kwa sasa wakiwa na mtandao wa mashine za ATM zaidi ya 270 nchini kote.
“Mkutano wa umejumuisha benki wanachama taasisi za kifedha na pia makampuni yanayosaidia kuwezesha mabenki kupata huduma za kifedha katika kuhakikisha mteja wa benki moja anapata huduma ile ile katika benki nyingine bila kuwa na akaunti katika benki hiyo”, alisema Mariam.
Mmoja wa wadau wa Umoja Switch, Prof. Edson Lubuwa akizungumza katika mkutano huo alisema Umoja inasaidia sana katika kufikisha huduma za kibenki mbali sana kwa waliopo vijijini katika maeneo ambayo hakuna huduma za uhakika za kibenki hivyo akatoa wito kwa Umoja kujitahidi katika kuhakikisha huduma zinawafikia watu wengi zaidi.
No comments:
Post a Comment