Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imesema itaendelea kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa ndani ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko kwa mazao yao, ukosefu wa ujuzi wa kutosha juu ya mbinu za kisasa za kilimo na ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kupanua shughuli zao na kulima kibiashara.
SBL kupitia programu yake wa Kilimo biashara, inafanya kazi na wakulima zaidi ya 400 waliopo sehemu mbalimbali nchini ikiwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuwapatia mbegu bora bure, kuwaunganisha na taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kupanua shughuli zao, mafunzo ya msingi ya ujasiriamali pamoja na kuwahakikisha soko kwa mazao yao kwa kuyanunua kwa bei iliyo juu ya bei ya soko.
Hatua hizi zimewekwa wazi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa SBL Mark Ocitti wakati akitangaza udhamini wa wanafunzi 102 wanaosomea masomo ya Kilimo katika ngazi ya diploma katika vyuo vya ndani ambapo alisema ufadhili huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza wataalamu.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kampuni ya SBL tayari imeshatoa ufadhili kwa wanafunzi 208 tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2020. Ocitti alisema, “Ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaonufaika na ufadhili wa masomo chini ya mpango wa Kilimo Viwanda ni sehemu ya uthibitisho wa nia yetu ya dhati ya kusaidia jamii ya kitanzania kwakuwa wanafunzi hawa wanatoka katika familia zenye kipato duni na pia sehemu ya mchango wetu katika kusidia maendeleo ya sekta ya kilimo’’.
Aliongezea, “ni matumaini yetu kuwa ufadhili huu utaleta matokeo chanya kwa maisha ya wanafunzi hawa ambao pia watatoa mchango muhimu kwa maendeleo ya sekta mama ya kilimo. Kupitia mpango huu wa Kilimo Viwanda, wanafunzi wanalipiwa gharama zote za masomo kwa kipindi chote cha masomo.”
Vyuo ambavyo vinanufaika na mpango huu ni pamoja na St. Maria Goretti cha Iringa, Kaole Wazazi cha Bagamoyo, Igabiro kilichopo Bukoba and Kilacha kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro. Wakuu wa vyuo vyote vinne walikuwepo wakati wa tukio la kutangaza kundi jipya na hawakusita kuiishukuru SBL kwa ufadhili huo ambao pamoja na kusaidia sekta ya kilimo, pia inawawezesha wanafunzi wanaotoka katika familia duni kupata nafasi ya kusoma.
Rebecca Juma ambae ni miongoni wa wanufaika wa ufadhili huu alisema ufadhili huu umekuwa ni mkombozi mkubwa sana kwake kutokana hali yake ya ulemavu. Alinukuliwa, ‘sikuwa na matumaini kabisa ya kupata nafasi ya kusoma kutokana na hali yangu, naishukuru SBL kwa kunipa nafasi hii’. Manafunzi walijawa na furaha kubwa kutokana na hali ngumu ya maisha waliyoishi na familia zao na kukata tamaa. Wengine hata kutokuwa na uwezo wa kulipa ada katika vyuo hivyo.
No comments:
Post a Comment