Akipokea miradi hiyo iliyo gharimu kiasi cha shilingi milioni 300, Rais Samia alisema Serikali inajivunia ushirikiano wa kimaendeleo baina yake na Benki ya CRDB. Aliongezea kuwa Benki hiyo imekuwa mfano mzuri wa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) katika kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya 2025.
Aidha, Rais Samia alisifu mafanikio ya Tamasha la Kizimkazi kwa mwaka huu 2021 ambalo lililenga katika kuhamasisha jamii kudumisha utamaduni na kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi kwa wananchi kwa kuonyesha fursa mbalimbali zitokanazo na tamaduni za Kitanzania. Tamasha hilo lilihusisha mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 500 juu ya ubunifu wa bidhaa za asili, elimu ya fedha na uendeshaji biashara, pamoja na michezo mbalimbali ya asili.
“Benki ya CRDB imetuonyesha kwa mfano kuwa tukiwekeza katika utamaduni wetu tutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa kutengeneza soko kwa bidhaa zetu za asili na Sanaa yetu. Kupitia Tamasha hili la Kizimkazi niiombe Wizara iweke mikakati ya kuanzisha matamasha ya utamaduni katika kila kanda hii itasaidia kukuza tamaduni za maeneo mbalimbali na kuchochea utalii,” alisisitiza Rais Samia.
Nsekela alisema Benki hiyo imedhamiria kwa dhati kusaidiana na Serikali kujenga uchumi jumuishi na kuwa utamaduni ni moja ya eneo ambalo Taifa likiwekeza vizuri linaweza kusaidia kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla. “Pamoja na vijielezi vingi vya neno utamaduni, sisi Kama Benki ya kizalendo tunaamini kuwa; utamaduni ni ujasiriamali, utamaduni ni utalii, utamaduni ni ajira, utamaduni ni uchumi.”
Alimwambia Mheshimiwa Rais, Benki hiyo pia inajivunia zaidi kuleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka 2014 Benki ya CRDB iliunganisha mfumo wake wa kielekroniki wa ukusanyaji mapato na mfumo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, ambapo ndani ya mwaka mmoja tu makusanyo yaliongezeka kwa zaidi 600%,” aliongezea.
Pamoja na mafunzo ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na Benki ya CRDB, Tamasha la Kizimkazi pia lilijumuisha usafi wa mazingira, mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na pete, kufua na kukuna nazi, nage, karata , bao, kuvuta kamba, resi za baskeli, resi za ngalawa, shomooo , na mashindano ya kuhifadhi Qurani.
Wananchi pia walipata fursa ya kupata chanjo ya UVIKO 19 ambayo itatolewa katika viwaja vya Kizimkazi Dimbani Mji Mpya, zoezi ambalo liliongozwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Ahmed Nassor Mazrui.
Kilele cha Tamasha la Kizimkazi kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment