- Faida baada ya kodi imefika TZS 205.5 bilioni ambacho pia ni kiwango kikubwa zaidi kwa sekta ya fedha Tanzania.
Akizungumzia matokeo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna amesema yametokana na utendaji imara uliojielekeza kukuza mapato na kuongeza ufanisi kwa kutumia teknolojia na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Kwa miaka mitano iliyopita, Taifa lilishuhudia ukuaji endelevu wa uchumi uliochangiwa na sera makini za fedha na kodi. Ni kutokana na mazingira haya wezeshi pamoja na utekelezaji makini wa mpango mkakati wa Benki tumefanikiwa kupata matokeo haya mazuri yaliyosaidia kukua kwa faida tuliyoipata,” amesema.
Faida ya Benki kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 40 kutoka TZS 211.1 bilioni iliyopatikana mwaka 2019 mpaka TZS 295.4 bilioni mwaka 2020 huku faida baada ya kodi nayo ikiongezeka kwa asilimia 45 kutoka TZS 142.2 bilioni mwaka 2019 hadi TZS 205.5 bilioni mwaka 2020 na kuifanya kuwa benki ya kwanza nchini kupata faida kubwa kiasi hicho.
Taarifa zake za fedha zisizokaguliwa pia zinaonyesha faida hiyo imechangiwa na ongezeko la mapato ya biashara yaliyopanda kwa asilimia 15 na udhibiti wa gharama za uendeshaji ambazo ziliongezeka kwa asilimia mbili tu (2%) ndani ya mwaka huo.
Kutokana na mpango mkakati wa Benki wa kuongeza ufanisi wa utendaji na huduma za kidijitali, mapato mengine yaliongezeka kwa asilimia 19 kutoka TZS 224.0 bilioni mwaka 2019 hadi TZS 266.2 bilioni mwaka 2020 yakichangiwa zaidi na ongezeko la wateja waliotumia huduma mtandaoni. Katika kipindi hicho, mapato yatokanayo na riba yaliongezeka kwa asilimia 11 kutoka TZS 518 bilioni za mwaka 2019 hadi TZS 574.0 bilioni mwaka 2020.
Hata hivyo, tengo la mikopo chechefu liliongezeka kwa asilimia 19 kutoka TZS 100.4 bilioni mwaka 2019 hadi 119.3 bilioni mwaka 2020, mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa changamoto kubwa iliyoletwa na janga la corona. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kama msimamizi wa sekta ya fedha, ilitekeleza wajibu wake vizuri kwa kutoa mwongozo uliotoa nafuu ya ukwasi hata kurekebisha urejeshaji wa mikopo iliyotolewa kwa wateja hasa waliopo kwenye sekta zilizoathirika zaidi na janga la corona.
Kuthibitisha kwamba NMB ni benki inayochangia zaidi kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, thamani ya mali zake iliongezeka kwa asilimia nane na kufikia TZS 7.1 trilioni katika robo ya nne mwaka 2020 kutoka TZS 6.6 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupanda kwa thamani ya mali hizo kulitokana na ongezeko la amana za wateja kwa kiasi cha TZS 369 bilioni. Mikopo iliyotolewa kwa wateja iliongezeka pia na kufika TZS 4.31 trilioni sawa na asilimia 15. Mikopo hiyo iliongezeka kutoka TZS 3.76 trilioni zilizotolewa mwaka uliotangulia zikiwa ni juhudi za benki kukuza mikopo inayotoa kwa sekta binafsi. Kwa ujumla, amana za wateja zilipanda kwa asilimia saba kutoka TZS 4.9 trilioni mwaka 2019 mpaka TZS 5. Trilioni mwaka 2020 kudhihirisha imani waliyonayo wateja nchini juu ya Benki ya NMB.
Bi. Zaipuna amesema mafanikio hayo yanatia moyo na ni uthibitisho wa uwajibikaji wa wafanyakazi wa Benki ya NMB, utekelezaji na usimamizi wa mpango mkakati, kuungwa mkono na wadau mbalimbali pamoja na imani waliyonayo wananchi na wateja wengine sokoni.
“Tukiendelea kutekeleza na kusimamia mpango mkakati wa biashara yetu, Benki imejielekeza katika kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wateja tukiongozwa na kuzielewa changamoto zao, huduma za kimtandao na uendeshaji wa shughuli zetu za ndani kidijitali zaidi ili kutufanya tuendelee kuwa juu wakati wote,” aliongeza.
Kwa mwaka 2020, mafanikio ya Benki ya NMB yameifanya itambulike na kupata tuzo za kimataifa ikiwamo ya Benki Salama Zaidi Tanzania iliyotolewa na Jarida la Global Finance, na kunyakua tuzo ya Benki Bora Tanzania iliyotolewa na Jarida la Euromoney kwa mwaka wa nane mfululizo. Ikihudumia takriban asilimia 22 ya wateja wote wanaotumia huduma za benki nchini na kupokea amana zao, NMB ndio yenye mizania mikubwa zaidi katika sekta ya fedha na inayoongoza kwa kupata faida kubwa nchini.
“Tunawashukuru wateja wetu, wafanyakazi, wanahisa, Serikali ya Tanzania, Benki Kuu pamoja na wabia wetu wa kimkakati kwa ushirikiano wanaoendelea kutupatia,” amesema Bi. Zaipuna.
No comments:
Post a Comment