Dar es Salaam, Juni 4, 2020 - Wateja wa DStv wanauanza mwezi huu wa Juni kwa habari njema za kurejea kwa michezo mbalimbali kote ulimwenguni iliyokuwa imesitishwa kwa miezi kadhaa kutokana na janga la COVID-19.
Kampuni ya MultiChoice Tanzania imethibitisha rasmi kuwa wateja wake wa kisimbuzi cha DStv wataanza kushuhudia michezo mubashara kupitia kuanzia katikati ya mwezi Juni ambapo michezo mingi iliyositishwa ikiwemo ligi kubwa na maarufu ulimwenguni kama ile ya Uingereza – Premier League, ya Italia – La Liga na ya Hispania – SerieA zinarejea na hivyo kuonyeshwa mubashara kupitia SuperSport kama ilivyokuwa hapo awali.
Akitangaza rasmi kurejea kwa michezo hiyo ndani ya DStv, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso, amewataka wateja wa DStv ‘kukaa mkao wa kula’ kwani ile burudani waliyoikosa kwa miezi michache sasa imerejea “Tunafurahi kuona kuwa michezo inafunguliwa sehemu mbalimbali duniani, na sisi kama vinara wa kuonyesha michezo hiyo, tayari tumejipanga kikamilifu kuwaletea wateja wetu burudani kabambe kupitia runinga zao”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MultiChoice Tanzania, kwa upande wa Kandanda, mashabiki wana kila sababu ya kusherehekea kwani ligi kubwa na maarufu barani ulaya na duniani kote zinarejea. Premier League, La Liga na Serie A zote zimethibitisha kurejea mwezi huu wa sita ambapo La Liga itaanza kutimua vumbi ndani ya SuperSport jioni ya Alhamisi Juni 11 ambapo watani wa jadi wa Seville, yaani Sevilla na Real Betis wataumana vikali. Kurejea kwa La Liga kutashuhudia mchuano wa aina yake kati ya Barcelona and Real Madrid wanaoongoza ligi hiyo kwa tofauti ya point mbili tu.
Shughuli pevu itakuwa nchini Uingereza kwenye Premier League, itakayovuruma kuanzia Juni 17 kwa kuliwa viporo viwili – Manchester City watakaoumana na Arsenal huku Aston Villa wakipigana ngeta na Sheffield United.
Macho na masikio ya washabiki wa soka duniani yataelekezwa kwa vinara wa ligi hiyo – Liverpool ambao wanahitaji ushindi katika mechi mbili tu watangazwe mabingwa wa msimu huu. Kibarua chao cha kwanza kitakuwa dhidi ya Everton mechi inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua kwani bila shaka yoyote Everton hawatakubali kirahisi kuwa daraja la Liverpool kuelekea kwenye ubingwa!
Serie A nayo haijaachwa nyuma ambapo Juni 19-21 kutakuwa na ‘patashika nguo kuchanika’ wakati vinara wa soka nchini humo watakapopigana vikumbo kuliwania kombe hilo. Bingwa mtetezi Juventus ana pointi moja tu mbele ya Lazio ambayo msimu huu imeonekana kuwa timu matata sana kwenye ligi hiyo ya Italia. Internazionale nayo si ya ‘kuchukuliwa poa’ kwani inaweza kupindua meza ikiwa itafanya vizuri katika michezo zake iliyosalia.
Kwa wateja wa DStv, kinachorejea siyo Kandanda tu, bali michezo mingine kedekede hivyo watazamaji wa SuperSport wajiandae kwa burudani isiyo kifani. Michezo mingine maarufu kama Rugby, Golf, Riadha, UFC na mieleka – WWE yote inarejea kwa kishindo kikubwa.
“Kwa kurejea kwa michezo hii mubashara, bila shaka yoyote SuperSport itaendelea kuwa kitovu cha michezo na burudani kwa wapenda michezo wote hapa Tanzania na tunawahakikishia kuwa tutaendelea kuwapatia burudani nyingi kadiri iwezekanavyo huku pia tukiendelea kumwaga ofa kedekede kwa wateja wetu wa DStv” alisisitiza Jacqueline.
Kwa maelezo zaidi kuhusiana na huduma za DStv tembelea www.dstv.com. Pia unaweza kupata uduma za DStv popote ulipo kwa kutumia app ya DStv Now. Kujiunga and DStv piga 0659070707.
No comments:
Post a Comment