Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa benki ya NMB, Abdulmajid Nsekela. |
Miaka miwili iliyopita, Benki ya NMB ilianzisha huduma ya NMB Wakala ili kuwafikia watu wenye akaunti za benki na wasio na akaunti kote nchini. Tangu hapo, imekuwa ni huduma ya kipekee ambayo imefikisha huduma za kibenki karibu zaidi ya wateja.
Tulipata fursa ya kuzungumza na Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa benki ya NMB - Abdulmajid Nsekela ambaye anaeleza safari ya NMB Wakala ndani ya benki na jinsi zilivyosaidia kufanikisha ajenda ya nchi ya utoaji wa huduma za kifedha kwa watu wote.
Swali. Nini majukumu ya NMB Wakala katika kuleta mapinduzi ya huduma za kibenki nchini?
Kwa asili, huduma za kibenki zimekuwa zikihusishwa na ‘matawi’ ambayo NMB imeitekeleza kwa mafanikio makubwa. Tunayo matawi katika kila wilaya hapa nchini. Matawi yamekuwa sehemu ya kawaida watu wanapohitaji kupata huduma za kifedha lakini tumebaini kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za kijamii na kiuchumi katika ngazi za chini zaidi ya wilaya ambazo tunahitaji kuzipelekea huduma za kibenki. Pia, Ripoti ya Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha (FSDT) ijulikanayo kama Finscope ya mwaka 2017 inaonyesha kwamba kuna takriban Watanzania milioni 7.9 ambao hawana akaunti katika benki lakini wanao uwezo wa kiuchumi kama walivyo wale wenye akaunti na wanafanya shughuli za kiuchumi ambako mzunguko wa fedha taslimu haupo katika mfumo rasmi wa sekta ya fedha.
Kwa sababu hii, tunao mtandao wetu wa NMB Wakala ambao unasaidia matawi yetu kwa kutoa huduma za kibenki karibu zaidi na wateja wetu na hata kwa wasio wateja wa NMB. Pia kuna suala la muda wa kutoa huduma katika matawi ambako benki nyingi zinafungwa saa 11:00 jioni, ambapo biashara nyingi bado zinaendelea. Biashara hizi zinahitaji usalama wa fedha na huduma za miamala; NMB Wakala imetoa suluhisho kwa kutoa huduma za kifedha baada ya saa hizo.
Swali. Ni kwa namna gani NMB Wakala inafaa katika dira ya benki ya kuwa mshirika bora zaidi katika huduma za kifedha nchini?
Dira ya NMB ni kuwa benki inayotoa huduma bora zaidi za kifedha nchini. Kwa miaka mingi tumekuwa tukitoa huduma zetu za kibenki kupitia matawi yetu zaidi ya 220 na mtandao wa mashine za ATM zinazofika zaidi ya 800 nchini kote. Benki pia imewekeza katika teknolojia ili kukidhi matakwa ya wateja kupitia ubunifu mbalimbali wa huduma za kidigitali kama NMB Mobile ambayo inatoa huduma za kibenki kupitia simu za mkononi, huduma za kibenki kwa intaneti, taarifa zaidi KYC na Akaunti ya Chap Chap. Kama benki, tunaamini kwa dhati kwamba tutaweza kuwafikia Watanzania walio wengi kwa njia rahisi zaidi na gharama nafuu kupitia tekinolojia ya digitali. Ni katika mipango hii, NMB Wakala inaongeza uwezekano wa benki kufikia dira yake ya kuwa mshirika bora zaidi katika kutoa huduma za kifedha kwa kila Mtanzania.
Swali. Tuambie huduma ipi ya NMB Wakala inayovutia wateja wa NMB na wale ambao sio wateja wa NMB
Mawakala wetu wote wanaonekana kirahisi na wanatambulika kirahisi wakiwa na mabango yenye kuonyesha NMB Wakala. Huduma zinazotolewa ni pamoja na:
Kuweka fedha, Kutoa fedha, Kuuliza salio na taarifa fupi, Pia, kupitia NMB Wakala unaweza kulipa deni, ada ya shule/chuo, kununua LUKU, kununua muda wa maongezi kwa mitandao yote ya simu, kulipia TV, bili za maji,faini za polisi, tiketi za ndege na huduma nyingine nyingi.
Tumeona pia mchango mkubwa wa NMB Wakala katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kukusanya KODI; wateja wote, wa NMB na wasiokuwa wa NMB wanaweza kulipa kodi za aina mbalimbali kama za Serikali za Mitaa, Kodi ya Majengo, Tozo ya Ardhi, TPA n.k. kwa kutoa tu kumbukumbu ya namba ya malipo kwa mawakala. NMB Wakala inatoa wigo mpana kwa kila mtu kufanya malipo bila usumbufu wowote.
Swali. NMB Wakala imepata mafanikio gani tangu kuanzishwa kwake miaka miwili iliyopita?
Hivi sasa tuna mawakala 6,000 wa NMB Wakala nchi nzima jambo linaloifanya NMB kuongoza katika soko la huduma za Uwakala wa Kibenki. Hii imetoa ajira kwa watu 6,000 ambao nao wameajiri watu wa kuwasaidia katika biashara zao za kila siku.Pili, takriban nusu ya wateja wa benki wanatumia NMB Wakala kufanya miamala mbalimbali ya mahitaji yao ya kifedha na zaidi ya wateja 300,000 wasio na akaunti NMB, kwa mwezi wanafurahia huduma mbalimbali za malipo kupitia NMB Wakala,nazo zipo karibu nao hivyo kupunguza gharama za ufanyaji wa miamala na muda. NMB Wakala imetoa fursa na kupanua wigo kwa watu binafsi ambao wanataka kuweka fedha zao benki baada ya saa za kazi kwa matawi ya benki (ambayo kwa kawaida hufunguliwa saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni). Hii imeongeza mchango wa zaidi ya asilimia 30 ya uwekaji amana unaofanywa kupitia njia hii.
Swali. Nini kinachoitofautisha NMB Wakala na wakala mwingine wa taasisi yoyote ya kifedha Tanzania?
NMB tumepiga hatua kubwa zaidi katika kuhakikisha mawakala wetu wanakua kibiashara; tunawapa mafunzo ya jinsi ya kukuza biashara zao; marupurupu hayana kifani. Tunawaona mawakala wetu kama wenza katika biashara kwa hiyo pia tunawapa mafunzo ya jinsi gani wanaweza kukuza biashara zao kwa kutumia fursa ya wateja wengi wanaokwenda kwao katika biashara yao ya msingi, hivyo kukuza mauzo ya biashara zao. Inapokuwa lazima, tunapeleka timu yetu ya mauzo katika baadhi ya NMB Wakala ili wawape mafunzo ya jinsi ya kutoa baadhi ya huduma za kibenki kama kufungua akaunti, kuweka fedha na kutoa.
Swali. Somo gani tunalopaswa kujifunza kutoka nchi nyingine kuhusu masuala ya Uwakala wa Kibenki?
Kama inavyofahamika, uwakala wa kibenki ni dhana mpya Tanzania. Tumejifunza mengi kutoka katika nchi kama Kenya na nyingine katika ukanda huu ambazo zimetoa huduma hii ya uwakala wa kibenki kwa muda mrefu. Kwa Tanzania, dhana hii bado inakumbana na changamoto kadhaa; kwa mfano, kuna changamoto ya usalama. Hata hivyo, jambo zuri ni kwamba idadi kubwa ya Wakala wanawekea biashara zao bima.
Swali. Kwa mtazamo wako, unaionaje hali ya baadaye ya NMB Wakala?
Hali ya baadaye ni kupungua kwa biashara inayotegemea kufanywa katika majengo na njia mbalimbali za kidigitali zikisaidiwa na uwakala wa kibenki kutamalaki. Tunatarajia kufanya vyema katika soko. Tutaendelea kuongeza uelewa ili kuhakikisha kwamba kila mmoja anakuwa na ufahamu mkubwa wa matumizi ya huduma mbalimbali zilizobuniwa na NMB ikiwamo NMB Wakala, NMB Mobile kuweka fedha na pia kufanya miamala karibu zaidi na majumbani kwao na popote kadri wapendavyo.
Swali. Una ujumbe gani kwa wateja wa NMB na Umma kwa ujumla kuhusu NMB Wakala?
Ni matumaini yangu kwamba Watanzania watazitumia huduma za NMB Wakala kama benki zilizo ‘karibu’ nao. Waziamini, wajisikie huru na wafanye miamala na biashara na mawakala wa NMB Wakala; wakati wowote mteja anapokuwa na Wakala aelewa kwamba hicho ni kituo cha huduma cha NMB ambacho pia kinatambuliwa na Benki Kuu ya Tanzania. Pia kwa yeyote anayetaka kushirikiana na NMB kama Wakala tunamshauri kutembelea tawi letu lililo karibu au tupigie kupitia simu ya bure namba 0800 002 002 kwa maelezo zaidi.
No comments:
Post a Comment