Watanzania walioko nje ya nchi wametuma zaidi ya dola milioni 25 katika akaunti za Tigo nchini Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja, kwa kutumia huduma ya WorldRemit au tovuti.
Desemba 2017, Dar es Salaam na London: Huduma ya kuhamisha fedha kidigitali inayoongoza WorldRemit na Kampuni ya kidigitali Tigo Tanzania wameshuhudia ukuaji wa kasi wa huduma za kuhamisha fedha kwenda katika akaunti za fedha za simu za mkononi nchini Tanzania, taarifa zimebainisha.
Katika kipindi cha miaka miwili cha ushirikiano baina ya kampuni hizi, huduma ya Tigo imebainika kuwa ndiyo huduma ya kutuma fedha inayokuwa kwa kasi zaidi miongoni mwa washirika wa WorldRemit.
Huduma hii inawawezesha Watanzania katika zaidi ya nchi 50 kutuma fedha kwenda katika akaunti za fedha za simu za mikononi kwa haraka. Wamiliki wa akaunti za fedha za simu za mkononi pia wanakuwa na uwezo wa kutuma fedha ndani ya nchi, kununua muda wa maongezi, kulipia ankara au kutoa fedha taslimu kupitia mtandao mkubwa wa mawakala wa Tigo.
Licha ya Tanzania kutajwa kuwa ni moja ya nchi ambayo ina gharama kubwa sana kutuma fedha miongoni mwa nchi za Afrika, huduma hii maarufu inapunguza gharama za utumaji wa fedha wakati huohuo ikifanya mchakato wa kutuma fedha kuwa wa haraka na salama zaidi.
Upokeaji wa fedha unachukua nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania. Mwaka 2015 nchi ilipokea zaidi ya dola milioni 400 fedha kutoka nje ya nchi, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
WorldRemit ni mfumo wa kidigitali wa kwanza unaotumia simu za mikononi kutuma fedha unaowaruhusu wahamiaji wanaofanya kazi nje ya nchi kutuma fedha kwa kufuata hatua chache moja kwa moja katika simu zao za mkononi bila kutembelea au kusimama katika foleni kwa mawakala. Kampuni inawajibika kwa 74% ya fedha zote zinazotumwa kupitia mfumo wa kutuma fedha kimataifa kwenda katika huduma za fedha za simu za mikononi.
Andrew Stewart, Mkuu wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika kutoka WorldRemit, alitoa maoni yake na kusema: “Ushirikiano wetu na Tigo unatoa nafasi zaidi kwa mamlilioni ya watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi kuwa na mbinu mbadala ambayo ni rahisi na salama ya kuwasaidia marafiki na familia zao pasipo kupanga foleni kwa mawakala wa kutuma fedha.”
“Mtanzania aliyehamia London, Stockholm au Sydney sasa anaweza kutuma fedha kuja nyumbani kwa haraka na kwa urahisi – ikiwa inasaidia kuhamisha fedha kwa haraka, usalama na uhakika zaidi kushinda mifumo ya kutuma fedha isiotumia mtandao wa simu inayotegemea mawakala wa kutuma fedha.”
Hussein Sayed, Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha za Simu za Mkononi wa Kampuni ya Tigo Tanzania, aliongezea: “Tigo tumejizatiti katika kutoa huduma kamili ya kifedha kwa wateja wetu. Kama sehemu ya malengo yetu ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kifedha, tunatazamia kuhudumia sio tu soko la ndani ya mipaka ya Tanzania bali pia kwa watanzania wote walioko nje ya nchi. Pamoja na hayo tunachukua hatua zote kuwapatia wateja wetu mfumo wa uhakika na salama kwa ajili ya kutuma fedha kimataifa.”
Kwa sasa wateja wa WorldRemit duniani kote wanafanya miamala 750,000 ya kuhamisha fedha kila mwezi kutoka katika zaidi ya nchi 50 kwenda kwa zaidi ya nchi wapokeaji 148.
Tembelea tovuti ya WorldRemit kwa taarifa zaidi kuhusu jinsi ya kutuma fedha Tanzania.
No comments:
Post a Comment